Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Yakataa Kuipokea Taarifa ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)

Taarifa ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyowasilishwa jana kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imekataliwa baada ya kubainika upungufu, ukiwamo udhaifu wa Sera ya Uwekezaji na kiasi cha fedha kilichowekezwa katika miradi iliyopita.

Uamuzi huo umekuja wiki moja baada ya kamati hiyo kuagiza kusimamishwa miradi yote mipya inayotarajiwa kutekelezwa na NSSF hadi Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kujiridhisha na utendaji wa mfuko huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengulwa alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambapo baada ya kupokea ripoti ya SSRA, alisema: “Kamati inaagiza kwamba SSRA isimamie miradi yote mipya inayotarajiwa kutekelezwa hivi sasa isimame haraka, ili iweze kujiridhisha na hesabu ambazo zimefanyika.”

Akizungumza baada ya kikao kati ya kamati hiyo na NSSF jana, Mchengulwa alisema mbali ya mfuko huo kutoonyesha gharama za uwekezaji katika miradi iliyopita, pia alisisitiza taarifa ya mfuko huo haijaonyesha miradi ambayo imeidhinishwa mwaka huu wala miradi ambayo iko kwenye hatua za mwisho za umaliziaji.

Mchengulwa alisema baada ya kubaini upungufu huo wanasubiri kwanza ripoti ya CAG iwasilishwe bungeni, Dodoma, Aprili 25, mwaka huu ili iweze kuijadili kwa kina.

“Baada ya kubaini mapungufu haya, tumeamua kusubiri kwanza Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya CAG ili nasi tuanzie hapo.Kwa sasa hatuwezi kupata taarifa ya CAG kwa sababu bado iko kwa Rais,” alisema Mchengulwa.

Mchengulwa, ambaye pia ni mbunge wa Rufiji alisema, “Sisi hatufanyi kazi kwa kusikiliza vyombo vya habari ila tunataka kujiridhisha baada ya kusoma ripoti ya CAG. Baadhi ya wanachama wanajitoa NSSF kwa sababu ya kashfa za ufisadi tunazoziona kwenye mitandao na magazeti.”

Kilichowashtua wabunge hao ni ripoti za vyombo vya habari kuhusu harufu ya ufisadi katika miradi mbalimbali ya mfuko huo; ardhi kuthaminishwa kwa kati ya Sh800 milioni na Sh1.8 bilioni kwa ekari moja; kampuni mbili kulipwa kwa kandarasi moja, mkandarasi kuzidishiwa malipo, na ukiukwaji katika utolewaji wa zabuni.

Miradi iliyoanzishwa na NSSF ambayo vyombo vya habari vimeonyesha kwamba ina harufu ya ufisadi ni wa ujenzi wa mji mpya wa Dege Eco Village, Kigamboni ambao thamani ya ekari moja ni Sh800 milioni; Arumeru ardhi imethaminishwa kwa Sh1.8 bilioni, mkandarasi wa ujenzi wa jengo la Mzizima ameongezewa Sh5 milioni.

Vyombo vya habari vilinukuu ripoti ya ukaguzi wa miradi uliofanywa na CAG pamoja na kampuni ya kimataifa ya Ernst & Young ambayo CAG amewasilisha kwa Rais John Magufuli, ingawa inadaiwa baadhi ya mambo yameondolewa baada ya majibu kupatikana kutoka NSSF.

Mchengulwa alisema baada ya ripoti ya CAG kuwasilishwa bungeni, kamati yake itamwita CAG kueleza ukaguzi wake na itawahoji pia SSRA kwa kushindwa kusimamia mfuko huo.

“Ni wazi kwamba wanachama wengi wa NSSF wameanza kujitoa kwa sababu ya taarifa mbalimbali wanazoziona kwenye mitandao. Sasa hali hiyo ikiendelea mifuko mingi itakufa na wananchi watakosa imani na mifuko hiyo,” alisema.

Aidha, Mchengerwa alisema kamati yake imeitaka serikali na SSRA kuangalia namna wanavyoweza kupunguza mifuko ya hifadhi kwani mingi, inafanya kazi moja na baadhi ya mifu- ko ina hali mbaya kifedha kiasi cha kushindwa kulipa wanachama.

Ofisi ya Makamu wa Rais
Wakati huohuo, kamati hiyo imebaini ukiukwaji wa sheria katika ujenzi wa  jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais ambalo tayari lina nyufa kuanzia chini mpaka juu na milango mibovu, jambo linaloashiria kwamba jengo hilo lina matatizo makubwa.

“Kuna baadhi ya kasoro katika kumbi za mikutano iliyopo katika jengo la makamu wa rais, kwa mfano, kumbi za mikutano zina milango midogo ya kutoka mtu mmoja, kama kuna dharura watu wanaweza kupata matatizo,” alisema Mchengulwa baada ya kutembelea jengo hilo.

“Nimeshaagiza Katibu wa Bunge aandike barua kumpa maelekezo CAG kuhusu ukaguzi wa jengo hilo. Wakala wa Majengo (TBA) wamejitetea hapa lakini tunataka kupata taarifa kamili ya value for money kutoka kwa CAG,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema sheria inaruhusu mkandarasi kulipwa asilimia 90 ya gharama zote na baada ya kukabidhi jengo analipwa asilimia 10 ya fedha zilizobaki, lakini alilipwa asilimia 98 ya fedha zote ambazo ni Sh8 bilioni na kubaki na asilimia mbili ambayo ni Sh200 milioni.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment