Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard
Swai ameiomba mahakama iingilie kati kile alichokiita rushwa ya kutisha
kwenye taasisi hiyo ya kutoa haki.
Wakili Swai alitoa wito huo
baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuachia huru mkurugenzi
mkuu wa zamani wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Geofrey
Mhando na wenzake wanne akiwamo mkewe Eva Mhando, katika kesi aliyokuwa
akiiendesha.
Katika kesi hiyo, Mhando, mkewe na maofisa wengine watatu
wa zamani wa Tanesco; France Lucas Mchalange, Sophia Athanas Misida na
Naftali Luhwano Kisinga, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi
mabaya ya madaraka, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka
za Serikali.
Hata hivyo, washtakiwa hao wameibwaga Takukuru
baada ya mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha
tuhuma dhidi yao.
“Haki haijatendeka na tunatarajia kukata rufaa,” alisema Wakili Swai alipozungumza na waandishi nje ya mahakama.
“Rushwa iliyopo mahakamani inatisha. Serikali inatakiwa kuingilia kati.”
Hata
hivyo, wakili huyo hakueleza rushwa hiyo ilifanyikaje katika kesi hiyo
ambayo iliendeshwa na taasisi hiyo iliyopewa dhamana ya kuzuia na
kupambana na jinai hiyo.
Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa
Aprili Mosi mwaka huu na Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema aliyekuwa
akisiliza kesi hiyo, lakini ikaahirishwa hadi Aprili 6, ambayo pia
ilisogezwa mbele hadi jana iliposomwa na Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Akisoma
hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Rusema, Hakimu Riwa alisema kwa mujibu
wa ushahidi, suala la msingi lilikuwa ni mkataba kati ya kampuni ya
Santa Clara Supply Limited na Tanesco.
Alisema katika mkataba,
Mhando, ambaye alikuwa mshtakiwa wa kwanza, alituhumiwa kutumia madaraka
yake vibaya kwa kushindwa kutangaza maslahi yake kuwa kampuni ya Santa
Clara ni ya Eva Mhando ambaye ni mkewe.
“Suala la msingi la
kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo anahusika katika utoaji wa zabuni na
nani aliyekuwa na maamuzi ya mwisho,” alisema Hakimu Riwa akisoma hukumu
hiyo iliyoandaliwa na Hakimu Rusema.
“Jibu la swali hilo ni kwamba Bodi ya Zabuni ya Tanesco ndiyo iliyohusika na mchakato huo.”
Hakimu
Riwa aliongeza kuwa miongoni mwa washtakiwa hao, hakuna hata mmoja
aliyekuwa mjumbe katika vikao vilivyoendeshwa na bodi hiyo ya zabuni,
wala kuitwa kuhudhuria mkutano wowote wa bodi hiyo.
“Kutokana na sababu hiyo, inawezekana vipi mshtakiwa huyu akatangaza maslahi yake katika mkutano ambao hakuhudhuria?”
Kuhusu
suala la mshtakiwa huyo kujua kama Santa Clara inamilikiwa na mkewe na
watoto wake, alisema kuwa inawezekana asijue kama wana kampuni.
Alisema kuwa hakuna ushahidi kuwa mshtakiwa huyo aliulizwa swali lolote kuhusu kampuni hiyo.
Katika
kusisitiza hoja hiyo, Hakimu Rusema katika hukumu yake hiyo alitoa
mfano kuwa mwanamke anaweza kufungua akaunti kwa siri benki na akaweka
fedha kisha mumewe asijue.
Kuhusu suala la mshtakiwa wa pili,
Eva, kughushi nyaraka na kuziwasilisha Tanesco, alisema hakuna ushahidi
wowote unaoonyesha kuwa alifanya kosa hilo na kwamba aliyesaini nyaraka
hizo ni mtu mwingine ambaye hata hivyo hakushtakiwa.
Wakati wote
Hakimu Riwa alipokuwa akisoma hukumu hiyo, baadhi ya watu ambao
wanasadikiwa kuwa ndugu wa washtakiwa hao, walionekana wakifanya ishara
ambazo zilionyesha wanamuomba Mungu.
Baada ya hukumu hiyo na
kuachiwa huru, Mhando alionekana kutoamini na alipotoka mahakamani,
alielekea moja kwa moja kwenye gari lake na kukataa kuongea na mtu
yeyote.
Hali hiyo ilionekana kuwatia hofu ndugu zake ambao
baadhi walimshauri asiendeshe gari, badala yake aendeshwe kwa kuhofia
kuwa kwa hali aliyokuwa nayo angeweza kusababisha ajali.
“Msimuachie
aendeshe, Mhando kaa kiti cha nyuma,” alisema mmoja wa ndugu zake.
Mhando alikubali na kuhamia kiti cha nyuma kisha mkewe naye aliingia
kwenye gari hilo na kuondoka viwanja vya mahakama.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 26, 2014 na kusomewa mashtaka na Wakili Swai.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment