Mfanyabiashara Said Lugumi
Stori: Elvan Stambuli na Makongoro Oging’, UWAZIDAR ES SALAAM: Sakata la mkataba kati ya Jeshi la Polisi Tanzania na Kampuni ya Lugumi Enterprises wa kufunga vifaa 108 vya kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi, limezua balaa lingine kufuatia madai kwamba, maofisa wa polisi wameanza kupita katika vituo wilayani na mikoani kukagua na kuunganisha mitambo hiyo ili iweze kufanya kazi.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa, zoezi hilo limeanza huku kukiwa na usiri mkubwa.
Habari kutoka makao makuu ya polisi zinasema kuwa, maofisa wa polisi walitawanywa vituo mbalimbali nchini wakifuatilia kwa karibu suala hilo ambalo linalitikisa vichwa vya viongozi serikalini.
Aidha, gazeti hili likiwa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Pwani, Ijumaa iliyopita lilishuhudia maofisa wa polisi wakiwa na wataalam kutoka makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar na kuambiwa walikwenda kwalengo la kuunganisha mashine hizo ili zianze kufanya kazi.
Baadhi ya polisi kituoni hapo waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwa kuwa siyo wasemaji, walidai kuwa kutofanya kazi kwa mashine hizo kulizorotesha shughuli za upelelezi hasa namna ya kuwatafuta wahalifu sugu wanaofanya uhalifu mkoa mmoja na kuhamia mwingine bila kujulikana.
Wakifafanua umuhimu wa mitambo hiyo, polisi hao walisema mhalifu, hasa jambazi anapokamatwa katika kituo chochote cha polisi, akifikishwa wilayani au mkoani hupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole na kuingizwa katika mtandao, hivyo kuwa rahisi kujua kama alishawahi kufanya uhalifu popote nchini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Bonaventura Mshongi alipoulizwa kama amepokea ugeni wa polisi kutoka makao makuu kwa ajili ya kufuatilia mashine hizo, alikiri kupata wageni ofisini kwake. Hata hivyo, hakuwa tayari kufafanua walichokifuata.
Tayari bunge limeunda kamati ndogo yenye wabunge tisa iliyopewa kazi ya kuchunguza kwa kina mkataba huo, kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aeshi Hilary.
Hilary alisema kuundwa kwa kamati hiyo kumetokana na uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye ameielekeza kwenda kuchunguza kwa kina mkataba huo na kupewa siku 30 za kufanya kazi hiyo kisha taarifa itatolewa bungeni.
Kamati hiyo itawahoji mawaziri, viongozi wa jeshi la polisi waliopo na waliostaafu na wafanyabiashara waliotajwa pamoja na kampuni zilizoshiriki kufunga mashine hizo.
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alipotafutwa kwa njia ya simu na Uwazi, juzi (Jumapili), alisema hana taarifa hizo na badala yake akaelekeza atafutwe msemaji wa jeshi la polisi, Advera Bulimba ambaye mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, hakupatikana.
Mwaka 2011, Kampuni ya Lugumi ilipewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini ambapo inadaiwa imeshalipwa Sh. bilioni 34 kati ya bilioni 37, sawa na asilimia 99 ya malipo yote.
Hata hivyo, kuna madai kwamba ni vituo 14 tu vilivyofungwa mashine hizo huku mashine moja pekee ikiwa ndiyo inayofanya kazi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment