Mkurugenzi Mkuu Takukuru-Valentino Mlowola
Sakata
la kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh37 bilioni na Jeshi la
Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole
nchi nzima, sasa limetua Takukuru baada ya taasisi ya kupambana na
rushwa kuchukua faili lake la usajili.
Kampuni
hiyo ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga
mashine 14 tu kati ya 108 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa
asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.
Wakati
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikitaka nguvu itumike ili
Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo, utata umeibuka katika umiliki
wa kampuni hiyo kutokana na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya vigogo wa
Polisi na wanasiasa ni wanahisa wa Lugumi Enterprises.
Jana,
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela),
Frank Kanyusi alisema kuwa Takukuru inashughulikia suala hilo, huku
akibainisha kuwa kwa sasa Brela hawana takwimu za kina za kampuni hiyo.
“Kampuni
hii ilisajiliwa kihalali na kupewa cheti cha usajili. Ila ninachoweza
kukueleza kwa sasa ni kwamba jalada la usajili la Lugumi lipo Takukuru
kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kinyusi jana.
Kanyusi,
ambaye hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu usajili wa kampuni hiyo,
alisema: “Waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza maswali mengi kuhusu
suala hili ila kwa sasa hali ndiyo hiyo. Jambo hili lipo Takukuru.”
Alisema
kwa sasa kampuni zilizosajiliwa na Brela zipo 120,000 na zinakaribia
kufika 130,000 na kwamba kampuni lazima zitoe taarifa zake kila mwaka,
kinyume na hapo zinaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa.
Habari
za uhakika kutoka ndani ya Brela zilieleza kuwa taarifa za usajili wa
kampuni hiyo zilitoweka takribani miezi miwili iliyopita.
Mwandishi
alipofika katika ofisi za wakala huyo kwa ajili ya kupata ukweli wa
usajili, alielezwa na mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake
kuwekwa wazi kwamba ni vigumu kupata hilo jalada kwa sababu ya mvutano
ulioibuka.
Hata
baada ya kufuata taratibu za kupewa jalada hilo kwa ajili ya kupitia
masuala mbalimbali, alijibiwa kuwa jalada hilo halionekani ingawa
baadaye Kanyusi alisema limechukuliwa na Takukuru.
Sakata
la Lugumi liliibuka wiki iliyopita wakati PAC ilipokutana na Jeshi la
Polisi kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na
CAG.
Katika
hesabu hizo ilibainika kuwa mwaka 2011, Polisi iliingia mkataba na
Lugumi kwa ajili ya kufunga mashine hizo katika vituo 108 vya polisi kwa
gharama ya Sh 37 bilioni.
Hata hivyo, ilibainika kuwa kampuni hiyo imefunga mitambo hiyo kwenye vituo 14 tu, huku ikilipwa asilimia 99 ya fedha hizo.
Kutokana
na ukakasi huo, PAC ambayo ilibaini viashiria vya ufisadi katika
mkataba huo, iliagiza watendaji wa Polisi kuwasilisha taarifa za mkataba
huo pamoja na vielelezo vyake ili kamati hiyo iweze kuupitia na
kujiridhisha.
Lakini
hadi sasa Jeshi la Polisi halijawasilisha mkataba huo, jambo ambalo
huenda likazua mjadala mkali katika mkutano wa Bunge unaoanza Jumanne
ijayo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment