Waliofunga Mita za Mafuta Bandarini Dar Kikaangoni ...Ni wale Waliogundulika Baada ya Ziara ya Kushtukiza ya Waziri Mkuu

Kamati ya Miundombinu imeitaka Serikali kuchunguza kwa kina na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika na kufungwa mita za mafuta zilizopo Bandari ya Dar es Salaam, bila kufanya kazi kwa miaka mitano. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Norman Sigala alisema kuna haja ya Serikali kujiridhisha kwa umakini lengo la kufungwa kwa mita hizo na sababu ya kufungwa kwake, kisha ichukue hatua.

“Kamati yetu inatambua wajibu wake ikiwamo kuielekeza Serikali, kuishauri na kuikosoa bila uoga tulitembelea tukaona zile mashine moja ya mafuta ya dizeli tayari ilifungwa na inaendelea kufanya kazi, sasa hiyo nyingine Serikali inapaswa kwenda ndani zaidi kiuchunguzi na kuchukua hatua kali kwa yeyote aliyehusika,” alisema. 

Februari 12, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya ghafla kwenye Kitengo cha Upimaji Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta mita zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. 

Kutokana na hali hiyo, alimpa saa nne Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita. 

Akizungumzia kiwango cha fedha za bajeti ya Sh4 trilioni iliyotengwa kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alisema kamati yake inaridhishwa na kiwango hicho. 

Hata hivyo, alisema Serikali inapaswa kuongeza upembuzi katika uteuzi wa watendaji wa idara na taasisi zake, ili kuepusha vitendo vya ufisadi ambavyo vimekuwa vikigharimu fedha nyingi kutafunwa ama kupotea katika mazingira ya kutatanisha, hivyo kukwamisha juhudi za maendeleo. 

“Serikali ifanye uteuzi vyema wa watendaji wake kigezo cha uadilifu na uwezo wa kazi kiangaliwe kwa makini, huwezi kuzuia rushwa mahali ambapo kiongozi si mwadilifu, kamati inaishauri Serikali nafasi hizo zisitolewe kama zawadi,” alisema. 

Alisema wameridhishwa na utendaji wa baadhi ya viongozi wanaokaimu nafasi za ukurugenzi wa taasisi hivyo na wameishauri Serikali pia iwathibitishe watu hao ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi vizuri zaidi.

Akizungumza kuhusu bajeti, Dk Sigala alisema kamati yake imeridhishwa na mipango ya Serikali iliyoweka kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 kwa wizara hiyo inayolenga kuboresha miundombinu muhimu. 
“Serikali imetenga mafungu ya fedha kwa ajili ya kuboresha reli, barabara, viwanja vya ndege pamoja na kununua ndege nne, na kwa kuanzia imetenga Sh250 bilioni kununulia mbili za kuanzia katika mwaka huu wa fedha,” alisema. 

Alisema hata hivyo katika kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Bandari wameishauri Serikali kupunguza baadhi ya gharama ambazo zinakuwa zinatozwa na mamlaka hiyo, nia ikiwa ni kuwezesha wavutia wafanyabiashara na kumudu ushindani na bandari za nchi nyingine.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment