Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amelitaka Jeshi la Polisi nchini na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka
kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya
taifa.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana tarehe 29 Aprili, 2016 wakati
akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili
wafawidhi wa serikali wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na
Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa
Dodoma uliopo katika eneo la Tambukareli Mjini Dodoma.
Awali kabla ya kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi
Makamanda na Mawakili Wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto
zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa kufanya upepelezi na
kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za kuchelewesha kesi za
makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya
kucheleweshwa kwa kesi za hizo.
Kufuatia kutajwa kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi
kuhakikisha anawatafutia fedha kwa ajili ya kukabiliana nazo, lakini
ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri kwa kuwa taarifa
zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya
fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake
wa kazi.
Ametolea mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa
kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye
mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya
mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
"Oysterbay pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja
anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu
anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya
gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa
benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka investment na
Polisi wenu wakakaa pale. Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi,
nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction ninayoitaka mimi" Amesema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujipanga
kufanya kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya
serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na
wanasheria mahiri.
"Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi
mtangulize maslai ya nchi mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi
ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema wachache, panapokuwa na kesi
inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao wanasema dili limepatikana,
na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wana-collude Mawakili wa
serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude siku zote
serikali inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali
inashindwa, halafu siku hiyo unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote
serikali inapata kigugumizi" amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa
ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa Polisi
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa
wahalifu wa ujambazi.
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka
apelekewe mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo
hivyo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment