Ripoti
ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) inayohusu miradi
inayosimamiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imepelekwa
kwa Rais Dk. John Magufuli kwa ajili ya kuipitia.
Awali
ripoti hiyo ilitakiwa kuwasilishwa juzi kwenye Kamati ya Katiba na
Sheria ya Bunge, baada ya wajumbe wa kamati hiyo kuiomba, lakini
ilishindwa kuwasilishwa na viongozi wa NSSF kwa madai kuwa kuna tuhuma
za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi mbalimbali inayosimamiwa
mfuko huo.
Akizungumza
na wajumbe wa kamati hiyo juzi, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama, aliwaambia ripoti hiyo imetua
mikononi mwa Rais Magufuli, hivyo hawawezi kuipata hadi aisome na
kuiwasilisha bungeni.
“Kutokana na hali hii, kamati haiwezi kuipata ripoti hii hadi rais mwenyewe atakapoamua kuiwasilisha,” alisema.
Alisema kuna uwezekano mkubwa mjadala wa ripoti hiyo ukaendelea bungeni, baada ya Rais Magufuli kuipitia na kutoa maelekezo.
Vyanzo
vya habari kutoka ndani ya kamati hiyo jana vilisema kuwa baada ya
Waziri Jenister kutoa taarifa hiyo, wajumbe wa kamati walipinga na
kuwataka watendaji wa NSSF waiwasilishe kwenye kamati hiyo kwa sababu
wao ndio walioiomba ili waweze kuipitia na kuangalia utekelezaji wa
majukumu ya mfuko huo.
Baada
ya mvutano huo, Waziri Jenister alisisitiza taarifa alizonazo ripoti
ipo kwa Rais, hivyo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuipata hadi ipelekwe
bungeni au atoe maelekezo mengine kwa kuwa yeye ndie mwenye kibali hicho
kwa mujibu wa sheria.
Waziri
Jenister alipotafutwa kuzungumzia suala hilo jana, alisema wizara yake
haiwezi kulizungumzia kwa sababu liko mikononi mwa kamati.
Alisema kisheria ripoti ikifikishwa kwenye mikono ya rais, wizara haina mamlaka ya kujadili tena.
Wiki
iliyopita, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, wakati
akitoa majumuisho ya ziara walizofanya katika taasisi mbalimbali za
Serikali na wizara, alisema walibaini kuwapo upungufu katika taarifa ya
utekelezaji wa miradi mingi inayosimamiwa na NSSF.
Alisema
kutokana na kasoro hizo, kamati iliona ni vema ikapata ripoti ya CAG
ili ipitie na kujiridhisha kama miradi imetekelezwa au kuna harufu ya
ufisadi.
“Kamati
imebaini kuwepo nyumba nyingi zilizojengwa na NSSF ambazo hazikaliwi na
watu, hali iliyotutia shaka. Inaonekana baadhi ya watu wamenufaika na
miradi hii.
“Tunaamini miradi hii haijawanufaisha wanachama wake bali watu wachache, ndiyo maana tumeagiza ripoti ili tuipitie,” alisema Mchengerwa.
Alisema
kutokana na hali hiyo, wameagiza kusimamishwa miradi mipya ya shirika
hilo na kuiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA),
kuhakikisha inasimamia ipasavyo mifuko pamoja na kuangalia miradi
inayoanzishwa kama inawanufaisha wananchi na Serikali kwa ujumla.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment