RPC Apiga Marufuku ‘Vigodoro’

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Bonaventura Mshongi
Stori: Makongoro Oging’, UWAZI
PWANI: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Bonaventura Mshongi (pichani) amepiga marufuku ngoma za kukesha zinazopigwa na makabila mbalimbali mijini, maarufu kama vigodoro katika mkoa wake, akidai zinachangia matukio ya kihalifu.

Katika mahojiano maalum ofisini kwake Kibaha, mwishoni mwa wiki iliyopita, kamanda huyo alisema yeye pamoja na viongozi wenzake wa mkoa, wamekubaliana kutoruhusu ngoma hizo, kwani uzoefu unaonesha baadhi ya wahalifu hujificha katika sherehe hizo, wakisubiri muda wa kufanya uhalifu ufike.

“Tunawategemea wananchi ndiyo maana tunawaasa kuendesha ulinzi shirikishi katika maeneo yao, wajenge tabia ya kuwa na daftari la makazi kuandikisha wageni, hii itasaidia kuzuia matukio ya uhalifu sehemu zao za makazi,” alisema kamanda huyo.

Hata hivyo, amewataka wamiliki wa baa kutofungua kabla ya muda ulioruhusiwa kisheria na amepiga marufuku uchezaji wa ‘pool table’ saa za kazi, pia amewaagiza wananchi kusalimisha silaha zao ili kuzikagua na kuwa upande wa wazazi wanaowakataza watoto wao kwenda shule kwa kisingizio cha udini, waache mara moja kwani jeshi hilo linafuatilia kwa karibu na watakaokutwa na hatia, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha, amewatahadharisha waendesha bodaboda kuwa makini wakati wa kubeba abiria, akiwataka kuacha kubeba ‘mishikaki’ kwani baadhi yao hawana nia nzuri na pia wavae kofia ngumu.

Kwa upande wa usalama barabarani, amewataka abiria kutoa taarifa polisi kwa madereva wakorofi wanaoendesha kwa kasi na amesema kuwa jeshi limejipanga vizuri kukabiliana na madereva hao.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment