Serikali Yashauriwa Kuwa na Hisa Kwenye Kampuni za Madini ili Kujua Mapato halisi Yanayoingizwa na Wawekezaji wa Kigeni

Serikali imeshauriwa kuwa na sehemu ya umiliki katika kampuni zinazochimba madini na gesi ili kujua mapato halisi yanayoingizwa na wawekezaji wa kigeni. 
Aidha, imeshauriwa kuzilazimisha kampuni hizo kurejesha nchini asilimia 60 ya mauzo yake, ili kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, pamoja na kuimarisha Shilingi ya Tanzania.

Ushauri huo ulitolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyestaafu, Ludovick Utouh pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa Uwazi katika mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (EITI), Jaji mstaafu Mark Bomani, wakati wa uzinduzi wa ripoti za kamati za mwaka 2013 na 2014 uliofanyika jana Dar es Salaam.

Akizindua ripoti hizo, Utouh alisema, Tanzania haijafaidika na rasilimali za madini, jambo lililosababishwa na kujiondoa kufanya biashara, hivyo kuzipa mwanya kampuni za kigeni kuendesha biashara bila uwazi kuhusu mapato zinazoyapata kutokana na mauzo ya madini.

“ Serikali iliangalie jambo hili na kulirekebisha, Serikali ya Botswana ina hisa kwenye migodi hiyo, hivyo wanakuwa na mwakilishi kwenye bodi jambo ambalo linakuwa rahisi kufuatilia mapato yanayopatikana, lakini sisi hapa tulijiondoa kwa madai kuwa Serikali haifanyi tena biashara,” alisema Utouh.

Alisema, Serikali ikifanya hivyo itaweza kupata mapato mengi zaidi kuliko ilivyo sasa, ambapo imejiondoa kabisa katika umiliki wa migodi ilhali rasilimali hizo ni za Watanzania.

 “Wawekezaji wanakuja na fedha na utaalamu, lakini sisi cha kwetu ni rasilimali, ni lazima tugawane nao na tuwe na mwakilishi kwenye bodi, badala ya kusubiri mrabaha unaotokana na faida anayopata mwekezaji. Huu utaratibu wa kuwaachia kila kitu sio mzuri,” alisema Utouh.

Naye Jaji Bomani alisema, Serikali inatakiwa kuzilazimisha kampuni zinazochimba madini nchini kurejesha asilimia 60 ya mauzo yake ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni. Alisema, kwa kufanya hivyo, Shilingi ya Tanzania itaimarika.

Alisema, hatua hiyo ikichukuliwa, sekta ya madini itakuwa imetoa mchango wake kwa pato la Serikali, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo. 

Alitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kupanua wigo wa wachimba madini kama vile wachimbaji wa kati na ambao pato lao linazidi Sh milioni 200, kwa mwaka ambao, alisema wanastahili kutoa mchango kwa pato la Serikali.

Alisema mpaka sasa ni kampuni kubwa tu zinahusika, lakini akasema umefika wakati wachimbaji wa kati nao waingizwe kwenye utaratibu huo. 

Alipendekeza kuwa umefika wakati sekta ya madini ipanuliwe hadi kwenye uchimbaji wa makaa kuiwezesha nchi kufaidika zaidi na shughuli za rasilimali hiyo, ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

EITI ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa mwaka 2002 na nchi mbalimbali zenye sekta ya madini. Linafanya ufuatiliaji juu ya sekta ya madini na gesi na kuona kama kuna uwazi katika biashara yake.

Tanzania ilijiunga na shirika hilo mwaka 2009. Kazi kubwa ya kamati iliyoundwa kushughulikia shughuli hizo hapa nchini ilikuwa ni kukusanya taarifa juu ya malipo ambayo kampuni za madini zilikuwa zinalipa serikali ya Tanzania na kuzilinganisha na mapato ambayo yalikuwa yamepokelewa serikalini na kutoa taarifa kila mwaka.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment