Shirikisho Vyuo Vya Elimu Ya Juu Wapongeza Uteuzi Wa Happi Na, Hamphrey Polepole Kuwa Ma-DC

Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu CCM, limepongeza Uteuzi wa vijana, Salum Happi na Humphrey Polepole kuwa wakuu wa wilaya uliofanywa hivi karibuni.
 
Katika pongezi hizo, Katibu wa Shirikisho hilo, Siraji Madebe, amewataka Happi (Kinondoni) na Polepole (Musoma) na Vijana wengine waliopatiwa nafasi mbalimbali, kuchapa kazi kwa bidii ili wasi kuendelea kuudhihirishia umma wa Watanzania kwamba Vijana wanao uwezo wa kushika madaraka.
 
Amesema, ni muhimu wajitume kwa sababu kutochapa kazi kwa bidii kutasababisha Umma uonekane umefanya makosa kuwaamini vijana, jambo ambalo halitarajiwi kutokea.
 
Pamoja na pomgezi hizo, Katibu wa Shirikisho hilo, amezungumzia masuala mengine ikiwemo changamoto dhidi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, zinazotokana na utendaji wa TCU na Bodi ya Mikopo. 

IFUATAYO NI TAARIFA KAMILI

UTANGULIZI;
Ndugu wandishi wa habari,awali ya yote nipende kutanguliza shukrani za dhati kwa Mwenyezi mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupatia uzima na Afya ili kutekeleza majukumu ya kitaifa.

Lakini pia Shirikisho la Wanafuzi  Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania linampongeza Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuendelea kutumbua majipu na Kuadabisha wote wanaokiuka Utaratibu, sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma hasa Wezi, Mafisadi, Wala rushwa na Watendaji wazembe wa Serikali, Tunamwomba Mh Rais kutorudi nyuma wala kuhofia chochote kwani Watanzania Zaidi ya Milioni 45 tupo naye katika maombi na kumuunga Mkono kwa dhati.
 
USHIRIKI WA VIJANA KATIKA NAFASI ZA UONGOZI
Ndugu wandishi wa habari,itakumbuka kuwa Serikali ya awamu ya nne (4) ya Mh Jakaya Mrisho Kikwete aliwateua Vijana wengi kupata fursa za Uongozi wa Nchi yetu

Katika awamu hii ya tano (5) pia chini ya MH Rais Dr John Pombe Magufuli , Ushiriki wa Vijana Umeshamiri na zaidi Tunaendelea kushuhudia wakishika nafasi Mbali mbali na tena za ngazi ya juu kabisa ikiwemo Mawaziri, Naibu Waziri, Wakuu wa wilaya na Wakuu wa Mikoa.
 
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya Juu Taifa, kwa niaba ya vijana wote Tunawapongeza Vijana wenzetu wote waliopata Uteuzi katika nafasi mbali mbali

Tunatoa pongezi za kipekee kwa uteuzi wa Vijana wenzetu uliofanywa na Mh Rais kwa ndugu Salumu Happi kuwa Mkuu wa wilaya Kinondoni na Humphrey Polepole  kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma hili ni heshima na Faraja kubwa kwa kuaminiwa na Taifa na kupewa majukumu ya kumuwakilisha Mh Raisi kwa ngazi ya hiyo ya wilaya.
 
 Ni dhahiri bila kigugumizi uteuzi huo umeendelea kuwa ishara kuwa  serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania inaimani kubwa na vijana katika kusimamia na kutekeleza majukumu kwa uaminifu na ufanisi mkubwa. 

Hii ikiwa ni kutokana  na uwezo na ufanisi wa hali ya juu
ulioonyeshwa na vijana mbalimbali waliopo na waliotangulia kuwa mfano katika taifa letu.
 
Tunapenda kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwa na imani na kuendelea kuwaamini vijana kumwakilisha kwenye nafasi mbalimbali za kuhakikisha mambo yanakwenda mbele.
 
 Nitoe mwito kwa vijana tuendelee kutunza imani hizi na uaminifu kwa viongozi bila ya kuwaangusha kwa ustawi wa maendeleo kwa Taifa letu. Mungu awaongoze kwa kila jambo na awaepushe kwa kila baya kwa ufanisi na Maendeleo ya Watanzania.
 
CHANGAMOTO ZA WANAFUNZI
Vile vile Shirikisho la wanafunzi la vyuo vya elimu ya juu Tanzania linatumia fursa hii kuzungumzia kidogo kuhusu changamoto dhidi ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya juu zinazotokana na wakala wa Udahili wa wanachuo nchini (TCU) na Bodi ya Mikopo.
 
 Kufuatia hizo chagamoto,Shirikisho la Wanafunzi Vyuo Vya Elimu juu Taifa linaiomba serikali kupitia bodi ya mikopo na TCU kuweza kutatua changamoto zifuatazo kwa wanafunzi;-

 TANZANIA UNIVERSITY COMISSION (TCU)
Kusajili vyuo visivyokuwa na sifa.
 Hii inapelekea wanafunzi kunyimwa haki yao ya msingi kama vile >kukosekana kwa mitaala inayokidhi haja na maadili ya somo husika, >kukosekana kwa madarasa ya kutosha kufundishia wanafunzi wote
> Kukosekana kwa wakufunzi wa kutosha na wenye sifa ya kufundisha masomo husika.
 
 Hata hivyo tatizo hili linapelekea kufungwa kwa vyuo hivyo mara  vinapoonekana kukosa vigezo jambo ambalo linaathiri wanafunzi katika masomo yao na hata kisaikolojia mfano St. Joseph Arusha baada ya chuo kufungwa wanafunzi waliathirika kwa kiasi kikubwa kwa sababu wengi walikuwa kwenye mpango wa five years (5) special programme ambao haukuwepo kwenye vyuo vingine.

Ombi kwa serikali
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya juu Taifa inaiomba Serikali kupitia bodi ya TCU ifatilie kwa kina na kuchukulia hatua vyuo vyote ambavyo havikidhi mahitaji ya wanafunzi ikiwemo na Mitaala. Pia tunaiomba bodi ijitahidi kujiridhisha kwa kina na chuo kabla ya usajili ili kuondokana na usumbufu wa kufunga chuo husika wakati wanafunzi wanaendelea na masomo

Kuwepo kwa tozo ya quality assurance fees.
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya juu Taifa, inaiomba TCU iangalie upya maana upande mwingine ni tatizo kwa wanafunzi.Hasa vyuo ambavyo vipo chini ya NACTE wanafunzi wengi wao hawana Mikopo na hata Wanafunzi Ambao wapo chini ya TCU, Tunaomba Mh Waziri wa Elimu pamoja na Bodi nzima ya TCU kukaa na kupitia Upya Hiyo tozo ili iweze kuondolewa kwa wanafunzi ambao wengi wao ni watoto wa maskini na wakulima wanaosoma kwa shida 

BODI YA MIKOPO
Kucheleweshwa kwa malipo ya mahitaji ya wanafunzi kama vile pesa ya chakula, malazi na special facult requirements.
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya Juu Taifa, Inasikitika kuona Bodi ya Mikopo inachelewesha  kutoa pesa za wanafunzi ndani ya muda husika na    Kushindwa kufika kwa wakati kwa pesa hizi kunapelekea migomo na uchochezi wa kukosekana kwa amani mashuleni, pia inarudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi kwa sababu  wengi wanashindwa kumudu gharama za masomo na mahitaji ya kila siku hivyo kushindwa kuhudhuria vipindi vya darasani kabisa na hivyo kutofanya vizuri katika masomo yao.

Ombi kwa serikali
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya juu Taifa, inaiomba serikali kupitia bodi ya mikopo kukamilisha malipo ya wanafuzi kwa wakati ili waweze kuwa na utulivu mashuleni na waweze kupata haki yao ya msingi katika kufanikisha masomo yao.

Kucheleweshwa kwa ada za wanafunzi wanaodhaminiwa na bodi.
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya juu Taifa, inaona hii ni changamoto kubwa inayopelekea kuyumba kwa huduma zinazopaswa kutolewa na chuo kwa ajili ya kufanikisha elimu bora kwa kila mwanafunzi. 
Huduma kama vile kuwalipa wakufunzi, kukarabati madarasa na kununua vifaa vya kufundishia na kufanyia majaribio kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi, zinashindwa kupatikana kwa wakati na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi katika masomo yao. Aidha bodi inalipa ada kidogo kidogo kwa wanafunzi wake mfano; bodi inaanza kulipa million 100 kwanza wakati pesa inayohitajika ni 1bilioni

Ombi kwa serikali
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya juu Taifa, Tunaiomba serikali kupitia bodi ya mikopo kukamilisha malipo ya ada vyuoni kwa wakati na kuachana na malipo kidogokidogo ili kuweza kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa ufanisi mkubwa.

Mikopo ya misimu kwa wanafunzi.
Shirikisho la Wanafunzi Elimu ya juu Taifa, inaona  Mikopo hii inatokana na kukosekana kwa utaratibu mzuri wa muendelezo wa malipo mwanafunzi anapoanza masomo kuanzia mwaka wa kwanza hadi anapohitimu. Wapo wanaofanikiwa kupata mkopo kipindi wanapoanza masomo na kushindwa kuendelea kupata mkopo katika muendelezo wa masomo hayo. 
Hii ni changamoto kubwa sana hasa kwa wanafunzi wasioweza kumudu gharama za mahitaji yao pindi wanapokuwa masomoni hivyo kupelekea kurudisha nyuma maendeleo yao na wengine kushindwa kuendelea na masomo.
 
Ombi kwa serikali
Kama bodi inaweza kudhamini mwanafunzi kuanzia mwaka wa kwanza mpaka atakapohitimu ifanye hivyo ili kuwawezesha wanafunzi hao kumaliza masomo yao na kupata elimu bora inayowastahili.
 
Ubaguzi katika utolewaji wa mikopo kwa wanafunzi.Bodi ya mikopo hutoa kipaumble kwa wanafunzi wa education na sayansi kuliko masomo mengine, hii ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wasiosoma masomo hayo kwa sababu inawanyima fursa ya kupata elimu hasa kwa wale wasiokuwa na uwezo mzuri kiuchumi.
 
Ombi kwa serikali Utolewe ufafanuzi wa kutosha kuhusiana na jambo hili ili wanafunzi waelewe sababu zinazopelekea jambo hili kuwepo.
 
Siraji Shaa  Madebe
K/KATIBU MTENDAJI MKUU
SHIRIKISHO LA WANAFUNZI
WA VYUO VYA ELIMU YA JUU
04/22/2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment