SIMBA SC NA COSTAL UNION NANI KUUNGANA NA YANGA,AZAM NA MWADUI?

TIMU ya Simba leo inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kucheza na Coastal Union Robo Fainali ya Kombe la FA. Mchezo wa leo licha ya Coastal Union kuonekana haifanyi vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini kocha wa Simba, Jackson Mayanja amesema Coastal Union sio timu ya kuidharau na lolote linaweza kutokea.
Mshindi wa mchezo wa leo ataungana na timu za Yanga, Azam na Mwadui FC, ambazo tayari zimetinga Nusu Fainali ya Kombe la FA. Mayanja alisema kikosi chake kimefanya maandalizi ya muda mrefu na kina imani ya kufanya vizuri.

“Tumejipanga kwa mchezo huo na tuna imani mambo yataenda vizuri, lakini sio kwamba tunajiamini asilimia kubwa, kwani Coastal sio timu ya kuidharau kwa sababu haifanyi vizuri, kwani lolote linaweza kutokea,” alisema.

Mayanja alisema wachezaji wake wanaendelea vizuri na tayari wale waliokuwa wamechelewa Hamisi Kiiza na Juuko Murshid wameungana na wenzao tayari kwa mchezo huo.

Kocha huyo alisema huenda wachezaji hao walichelewa kuungana na wenzao kwenye mazoezi kwa kuona kuwa kuna mechi ambayo sio ngumu mbele na kwamba katika mchezo hakuna timu ndogo zote hucheza kwa juhudi kuhakikisha zinafanya vizuri.

Simba inaongoza Ligi Kuu Tanzania bara ikiwa na pointi 57 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 53 ikiwa nyuma kwa michezo miwili ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 52 ikiwa nyuma kwa mchezo moja.

Coastal Union yenyewe inashika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16 ikiwa na pointi 19 katika michezo 26 iliyocheza. Bingwa wa Kombe la FA, ambalo pia hujulikana kama Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF-CC) mwakani.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment