Beki wa Yanga Kelvin Yondani.
MAPEMA wiki ijayo Yanga itarudiana na Al Ahly nchini Misri
katika mechi ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha wa Simba,
Jackson Mayanja amesema anaitakia mema Yanga lakini amemuonya beki wa
timu hiyo, Kelvin Yondani.
Mayanja raia wa Uganda, alisema anaweka uzalendo mbele kwa kuitakia
kila la kheri Yanga katika mchezo huo ila Yondani inabidi abadilike la
sivyo ataigharimu timu.
Katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, wikiendi iliyopita,
Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly inayonolewa na Martin Jol,
kocha aliyewahi kuinoa Tottenham Hotspur ya England.
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja.
“Naitakia mema Yanga kwenye mechi yao ya marudiano dhidi ya Al Ahly
ya Misri, ila namuonya Yondani kuhusiana na aina ya uchezaji wake kwa
wapinzani.
“Yondani kama hatoambiwa ukweli anaweza kuigharimu Yanga katika mechi
hiyo kwani anacheza kindava anapowania mipira ya juu na mpinzani na
kila mara anakuwa kama anapiga kiwiko.
“Sasa kule ni ugenini kama akiendelea kucheza hivyo usishangae kuona
Yanga ikipata tatizo la kucheza pungufu uwanjani na hapo ndipo matatizo
zaidi yatakuwa kwa timu yake, asipobadilika atapewa kadi nyekundu tu,”
alisema Mayanja. Kesho Jumapili Yanga inatarajiwa kuondoka nchini kwenda
Misri tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumanne ijayo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment