Mabeki Wakiri NGOMA ni Balaa!

Donald-Ngoma-vs-Josephat
Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma (kulia) akimtoka beko.
MARA nyingi Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amekuwa akilalamika kuwa waamuzi wa Ligi Kuu Bara wamekuwa wakimbeba mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma mbele ya mabeki kwa kuwapa kadi nyekundu ambazo anadai huwa haziwi halali.
Manara akaenda mbali kwa kusema, kadi hizo nyekundu ndizo zimekuwa msaada wa Yanga kushinda mechi zake kadhaa.
Kutokana na hali hiyo, Championi Jumamosi ili kujiridhisha limezungumza na mabeki ambao mpaka sasa wamelamba kadi nyekundu na wamekiri kuwa Ngoma hazuiliki kirahisi uwanjani.
Pia wachezaji na makocha wakongwe waliowahi kucheza ligi kuu, wamemzungumzia nyota huyo na kusema kadi ambazo amekuwa akisababisha ni halali.
Hadi sasa straika Donald Ngoma amesababisha kadi nyekundu nne katika mechi za Ligi Kuu Bara na moja Kombe la FA huku akisababisha penalti tatu.
Ngoma-3.jpg
Donald Ngoma akifanya yake na  Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Ngoma, raia wa Zimbabwe, hadi sasa amefunga mabao 14 katika Ligi Kuu Bara na mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pamoja na uhodari wake wa kufunga, gumzo sasa ni namna anavyoweza kutengeneza kadi nyekundu kwa timu pinzani ambapo baadaye Yanga hupata ushindi.
Mara nyingi Ngoma amekuwa akisababisha kadi nyekundu wakati ambapo Yanga ipo sawa na wapinzani wao na baada ya hapo huwa inashinda mechi zake.
Kadi alizosababisha;

LIGI KUU 
Abdi Banda –Simba
Februari 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, beki Abdi Banda wa Simba alimchezea rafu Ngoma na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kisha nyekundu na mwamuzi Jonesia Rukyaa katika dakika ya 25.
Wakati huo, Yanga ilikuwa haijapata bao. Baada ya Banda kutoka nguvu ya Simba katika kuzuia ilipungua na Yanga ikapata mabao mawili yaliyofungwa na Ngoma na Amissi Tambwe. Yanga ikashinda mabao 2-0.
Tumba Sued-Mbeya City
Desemba 26, 2015 hadi dakika ya 56 Yanga ilikuwa inaongoza mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City katika mechi ya ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar lakini beki wa Mbeya City, Tumba Sued alimpiga ngumi Ngoma na kutolewa kwa kadi nyekundu. Yanga iliongeza bao moja na ikashinda mabao 3-0.
NGOMA AKISHANGILIA GOLI (5)
Akishangilia na Thabani Kamusoko (kulia).
Shaban Sunza ‘Chogo’ -Kagera Sugar
Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga ilicheza na Kagera Sugar mechi ya ligi kuu na hadi zinakwenda mapumziko zilikuwa sawa kwa bao 1-1.
Ile kipindi cha pili kinaanza tu dakika ya 46, beki wa Kagera, Shaban Sunza alimchezea rafu ya pili Ngoma na kuonyeshwa kadi nyekundu. Baadaye Yanga ilipata mabao mawili na ikashinda 3-1.

Iddi Mobby-Mwadui FC.
Aprili 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kwa mara nyingine Ngoma alimsababishia kadi nyekundu beki wa Mwadui FC, Iddi Mobby dakika ya 70 wakati timu zao zikiwa sawa kwa bao 1-1.
Baada ya bao hilo, Yanga iliongeza presha na kupata bao la pili dakika ya 87, lililofungwa na Haruna Niyonzima, Yanga ikashinda mabao 2-1. 

KOMBE LA FA
Paul Ngalema- Ndanda FC
Machi 31, mwaka huu Yanga ilicheza na Ndanda FC katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA. Awali beki Ngalema alimchezea rafu Ngoma akaonyeshwa kadi ya njano lakini dakika ya 69 beki huyo alimchezea rafu Simon Msuva na kusababisha penalti iliyozaa bao la pili la Yanga. Yanga ikashinda mabao 2-1.
1
WASIKIE MABEKI;
Mobby wa Mwadui alisema; “Ngoma ni msumbufu sana anapokuwa na mpira usipokuwa makini atakuacha, ana nguvu na kasi, alinipa tabu sana kumkaba ndiyo maana kuna wakati ilinibidi nimtulize kwa rafu.
“Pamoja na kumfanyia hivyo bado hakuogopa, alikuwa anakuja kasi tu na matokeo yake akanisababishia kadi ya pili ya njano na mwisho wake nikapewa nyekundu, akiendelea hivi wengi watapata kadi nyekundu.”
Tumba wa Mbeya City, alisema: “Ngoma ana mbinu nyingi halafu ana nguvu na kasi, pia ni mjanja, mimi sikumchezea rafu ila nilimgonga na mkono usoni akatumia mbinu zake kumdanganya mwamuzi nikapewa kadi nyekundu.
“Mabeki wanatakiwa kuwa makini kwani usipomchezea rafu ataweka mazingira mengine ili mradi utolewe kama mimi.”
Naye beki wa Kagera, Chogo yeye alisema; “Yanga sijui wamempata wapi yule mchezaji, kama beki hauko fiti na makini lazima atakusumbua kwani ana nguvu na anajua kumiliki mpira, pia ana kasi ya ajabu.

“Siku ambayo nilikutana naye uwanjani tulipocheza na Yanga, nilipata kazi kubwa sana ya kumkaba, ikabidi nitumie mbinu ya kumchapa viatu ili nimpunguze kasi, lakini haikusaidia.”
Beki Ngalema wa Ndanda kwa upande wake alisema: “Tuache mzaha, yule Ngoma ni mchezaji mzuri sana ana juhudi binafsi za kupambana uwanjani ili timu yake ipate kile wanachohitaji.
“Ni mjanja, ukimgusa kidogo tu anaanguka na unaonekana umemchezea rafu halafu unapewa kadi, najipanga vizuri tukirudiana katika ligi asinisumbue.” 

PAWASA, LUNYAMILA NAO
Beki wa kati wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema: “Ngoma ni mjanja na beki yeyote asiyetumia akili lazima atapata shida kumkaba. “Anachokifanya wakati anawania mpira ni kuhakikisha kwanza anauwahi mpira na kuuficha miguuni mwake na kumuacha beki akiwa nyuma yeye akielekea golini, sasa beki asiyejua lazima atamchezea rafu na kusababisha kadi.
“Ngoma atawasumbua sana na timu zitafungwa sana kwa mtindo wake anaocheza, Yanga itapata penalti nyingi na ushindi pia.”
Kwa upande wake, winga wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila alisema; “Ngoma anajua kazi yake uwanjani, kadi alizosababisha ni halali, huyu (Ngoma) ana kasi sana pindi anapopata mpira. Mara nyingi anawazidi kasi mabeki ambao humchezea vibaya, mabeki wasipokuwa makini watakumbana na adhabu kila siku.”
NGOMA AKISHANGILIA GOLI (6)
MAKOCHA WAKONGWE
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Mshindo Msola, akimzungumzia Ngoma anasema; “Ngoma ni mchezaji mzuri, anayajua majukumu yake anayopaswa kufanya uwanjani, ndiyo maana anawasumbua sana mabeki na kujikuta wakimchezea faulo kila wakati.”
Naye Kocha wa JKT Ruvu, Abdallah Kibadeni alisema: “Simfahamu vizuri Ngoma, lakini taarifa zake nazipata kuwa ni mshambuliaji hatari mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao, namsubiri tutakapokutana kwenye ligi kuu.
“Ukiona mchezaji anatajwa kila wakati, basi ujue ni hatari kwani nasikia anajua kupambana na mabeki.” 

NGOMA MWENYEWE
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ngoma ambaye alisajiliwa na Yanga mwaka jana akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, alisema; “Najua nimekuja kufanya nini na nitahakikisha Yanga hawatajutia. Kuhusu mabeki kucheza hovyo, ni hali ya kawaida, huwezi kuwazuia na wajibu ni kupambana tu.” 

MTIBWA LEO
Leo Yanga inacheza na Mtibwa Sugar katika ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ni wakati mwingine wa kusubiri kuona nini kitatokea.
-GPL
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment