ZITTO Kabwe Aibua Mazito Bungeni: Ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti, Ufisadi wa Hati Fungani ya Sh1.2 Trilioni

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe jana aliibua mambo mazito bungeni wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Rais –Tamisemi na Utawala Bora, likiwamo la ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti kutokana Bunge kupitisha bajeti Sh23.7 trilioni huku Serikali ikija na bajeti ya Sh29 trilioni.

Mambo mengine yaliyobainishwa na mbunge huyo ni sakata la ufisadi wa hati fungani ya Sh1.2 trilioni katika Benki ya Standard ya Uingereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushindwa kutoa majibu ya uchunguzi wa miamala kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda Benki ya Stanbic.

Kuhusu bajeti, Zitto alisema kuna ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 katika mchakato wa bajeti ya mwaka 2016/17 kwamba kifungu cha 8 cha sheria hiyo kinaeleza namna ambavyo mfumo wa bajeti ya Serikali unapaswa kuwa.

“Vifungu cha 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinataka ‘mpango na miongozo ya bajeti’ ipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Februari kila mwaka. Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha Mpango wa Bajeti uliokuwa na Bajeti ya Sh23.7 trilioni,” alisema.

Alisema kiasi hicho ni tofauti na bajeti inayojadiliwa sasa ya Sh29.5 trilioni na kubainisha kuwa jambo hilo si utawala bora kwa maelezo kuwa utungaji wa bajeti umeainishwa kisheria na kama sheria hazifuatwi, ni vigumu hata Bajeti yenyewe kutekelezwa.

“Ili kurekebisha hali hii ni lazima Bunge likae tena kama kamati ya mipango na kupitisha upya viwango vya juu vya bajeti kabla ya mjadala wa bajeti kuendelea au angalau kabla ya kupitisha bajeti kuu, Juni 2016,” alisema na kwamba bajeti za taasisi hazimo kwenye vitabu vya bajeti ya Serikali kinyume na sheria ya bajeti.

Kuhusu ufisadi wa Sh1.2 trilioni, mbunge huyo alisema mwaka 2013, Serikali ilikopa fedha hizo kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank, kwamba mkopo huo wenye riba inayoweza kupanda umeanza kulipwa Machi mwaka huu.

Alisema mkopo huo utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana na kuongeza kuwa mkopo huo umegubikwa na ufisadi huku baadhi ya Watanzania wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani wakihusishwa na sehemu ya mkopo huo.

“Jambo la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Vilevile, waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Waliopo mahakamani ni wanaosemekana kutumika kupeleka rushwa. “Mjumbe kashtakiwa, lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.”

Alisema ana barua ya kundi la Watanzania zaidi ya 2,000 wakitaka benki hiyo ya Uingereza ichunguzwe katika suala hilo la hati fungani huku Takukuru ikitumia taarifa ya Taasisi ya Uingereza ya (SFO) katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hilo.

Alisema SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya benki hiyo ya Uingereza na kushangazwa na Tanzania kusaidiwa kesi hiyo na wataalamu kutoka nchi hiyo.

“Iwapo tutafanikiwa kuonyesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu, Tanzania itakuwa fundisho kwa kampuni ya kimataifa kwamba Afrika siyo mahala pa kuhonga na Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake na tutaokoa zaidi ya Sh2 trilioni katika deni la Taifa,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment