Wakati Mdhibiti na Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG) akisema Pride (Promotion of Rural Initiatives
and Development Enterprises) ni shirika la umma, Msajili wa Hazina,
Lawrence Mafuru anasema hana nyaraka zinazoonyesha shirika hilo kuwa la
Serikali bali anajua kuwa ni asasi isiyo ya kiserikali (NGOs).
Kauli
hiyo ya Mafuru imekuja siku chache baada ya CAG kutoa ripoti ya ukaguzi
wa hesabu za mwaka 2014/ 2015 ambayo inaeleza kwamba shirika hilo la
utoaji mikopo ni mali ya Serikali.
Kama ilivyo katika ripoti za
mwaka 2013/ 2014, safari hii CAG amesisitiza kwamba Pride ilianzishwa
Mei 5, 1993 chini ya Sheria ya Makampuni (CAP 212) kwa lengo la kutoa
mikopo midogo kwa wajasiriamali.
Ripoti zote mbili za CAG
zinabainisha kwamba fedha za kuanzishia taasisi hiyo zilitoka Shirika la
Maendeleo la Norway (Norad) kwa makubaliano baina ya Serikali za
Tanzania na Norway. Pia, Serikali ya Sweden ilijiunga kukifadhili chombo
hicho mwaka 2001.
Katika ripoti ya mwaka 2014/ 2015, CAG
anasema kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hazina ya uwekezaji wa
Serikali katika makampuni, kufikia Juni 30, 2008 hisa zote za Pride
zilikuwa zinamilikiwa na Serikali.
Lakini kuanzia siku hiyo, shirika hilo liliondolewa kwenye orodha ya mashirika ya umma.
“Uhalali
na sababu za kuondolewa kwa shirika hili katika orodha ya Msajili wa
Hazina hazikuweza kubainika. Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya
Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, kila Shirika la Umma linatakiwa
kuleta hesabu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
ajili ya kukaguliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kumalizika
kwa mwaka wa fedha. Hata hivyo, hesabu za Pride Tanzania hazijawahi
kuwasilishwa kwenye ofisi yangu kwa ajili ya ukaguzi kama inavyotakiwa
na sheria,” anasema CAG.
Lakini Msajili wa Hazina, Mafuru
alikuwa na maelezo tofauti na CAG. “Hatuna ‘document’ (nyaraka) yoyote
inayoonyesha kuwa Pride Tanzania Ltd ni shirika la Serikali. Kama
ulivyosema kwenye taarifa hiyo ya CAG, taasisi hiyo
ilianzishwa kwa sheria ya makampuni inayosimamiwa na Brela (Wakala wa
Usajili wa Biashara na Leseni),” alisema Mafuru.
“Serikali
inaweza kuanzisha kampuni kwa kuhamisha mtaji; mlipaji ambaye ni
Serikali atapeleka kiasi cha fedha kwa shirika lililoanzishwa cha Sh100
bilioni kupitia Benki ya Uwekezaji nchini (TIB).
“Kuna mashirika
yanayoanzishwa kwa matamko ya Serikali kama vile Brela, Ewura (Wakala
wa Udhibiti wa Nishati na Maji), TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa
Mawasiliano Tanzania). Kuna mashirika yanayoanzishwa kwa Sheria za
Bunge, nayo yanakuwa ya umma.
"Lakini Serikali haikuweka mtaji
Pride wala haikutamka, ndiyo maana kwenye ofisi hii (Msajili wa Hazina)
hakuna kumbukumbu yoyote.”
Msajili huyo alisema inawezekana Serikali iliidhamini taasisi hiyo wakati Norad ilipotoa mtaji kipindi cha kuanzishwa kwake.
“Sababu
ya Pride kupitia Serikali, inawezekana Norad hawakuwa na uhakika na
sekta binafsi. Serikali ilikuwa kama msimamizi tu, lakini haina hisa,”
alisema Mafuru.
Mkurugenzi mkuu wa Pride yenye makao yake jijini Arusha, Rashid Malima alisema Msajili wa Hazina ndiye mwenye majibu sahihi.
Malima
alisema Pride Tanzania ilindikishwa mwaka 1999 chini ya sheria ya
makampuni (Cap 1,2) ikiwa ni kampuni ambayo iko chini ya wadhamini
isiyokuwa na hisa.
“Sheria inatoa nafasi kwa anayetaka
kuandikisha kampuni kuangalia ni aina gani ya kampuni anayotaka
kuandikisha na inafuata sheria ipi ya uandikishwaji wake. Pride Tanzania
iko chini ya wadhamini ambao kimsingi sheria inazuia wao kuwa
wanufaikaji tofauti na kampuni yenye hisa ambayo wahusika ni
wanufaikaji,” alisema Malima.
Huku akinukuu ripoti ya CAG,
Malima alisema mwaka 2008 ilikuwa taasisi ya Serikali. lakini 2010
inaonyesha iliondolewa na CAG hana maelezo ya kutosha kwanini haipo
chini ya kampuni za Serikali zinazopaswa kukaguliwa na ofisi yake.
“Kimsingi
makampuni yote yanasajiliwa na Msajili wa Hazina na ndiye mwenye
kufahamu kwa usahihi hatua zote za taasisi au kampuni iliyokuwa ya
Serikali kuwa ya binafsi,” alieleza.
Kuhusu nani huwa anakagua hesabu zao, Malima alisema huwa zinakaguliwa na taasisi ya kimataifa ya Ernst & Young.
Mwenye
jukumu la kukagua hesabu za Serikali pamoja na mashirika ya umma ni
CAG, lakini kutokana na ukubwa wa jukumu hilo huwa anateua mashirika
kama Ernst & Young au Deloitte et Touche.
Akijibu maswali
bungeni mjini Dodoma Machi 30 mwaka jana kuhusu hadhi ya Pride, Naibu
Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema taasisi hiyo si ya kiserikali.
“Mheshimiwa
Spika, taasisi ya Pride Tanzania ni asasi isiyo ya kiserikali
iliyosajiliwa kama kampuni tarehe 5 Mei, 1993 chini ya wadhamini wasio
na hisa (Company Limited by Guarantee, Not Having Share Capital),
kulingana na Sheria ya Makampuni Cap, 212 ya mwaka 2012, ” alisema
Malima.
“Lengo la kuanzishwa kwa asasi hiyo ni kuwawezesha
walengwa wake kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa
kati sehemu za mijini na vijijini.
"Asasi hii ina mtandao wa jumla ya matawi 71 katika mikoa yote na baadhi ya wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar.”
Alikuwa
akijibu bungeni swali la Amina Mwidau aliyetaka kujua sababu za Pride
kupotea kwenye orodha ya taasisi za serikali ambayo iliiwekea dhamana
wakati ikianzishwa.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment