Rais John Magufuli ameagiza Koplo Deogratius Mbango kupandishwa cheo
baada ya kumdhibiti mke wa waziri mmoja wa Serikali yake aliyepambana na
askari huyo wa barabarani baada ya dereva wake kufanya kosa eneo la
Namanga jijini Dar es Salaam.
Koplo Mbango alikumbana na tukio
hilo baada ya dereva wa mke huyo wa waziri kusimama kwenye alama za
kuruhusu watembea kwa mguu kuvuka barabara na alilazimika kupiga simu
kituoni kupata maelekezo baada ya mama huyo kujitambulisha kuwa ni mke
wa waziri.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha
makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali, na wakuu
wa upelelezi wa mikoa na vikosi, kilichofanyika mjini Dodoma, Rais
Magufuli bila kumtaja jina alisema amemwonya waziri huyo na mkewe.
“Ebo!
Yule trafiki anajua kazi, mpandishe cheo. Na huyo waziri na mke wake
nimeshamwambia,” alisema Rais Magufuli, kwa mujibu wa taarifa ya habari
ya TBC1.
Licha ya polisi na Rais Magufuli kutotaja jina la
waziri huyo, mazungumzo kwa njia ya simu ambayo yamesambaa
yanaonyesha mwanamke huyo aliyekamatwa akijitambulisha kwa jina la
waziri mmoja mpya katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Majibizano ya polisi na mama huyo yanaonyesha kuwa dereva
wake alikamatwa baada ya kusimama katikati ya mistari ya pundamilia,
ambayo ni ishara ya kuvukia waendao kwa miguu.
Mazungumzo hayo
yaliyorekodiwa yanaanza wakati Koplo Deogratius alipompigia simu kamanda
wa trafiki wa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Awadh Haji na
kumueleza tukio lililokuwa mbele yake.
Kadhalika Koplo
Deogratius alimueleza RTO Haji kuwa wakati anataka kumuandikia faini,
dereva huyo alitaka kuondoa gari na mama huyo akamtukana.
“Huyu
mama akawa ananitukana… anasema yeye ni mke wa waziri. Nikamuambia hilo
ni kosa la dereva, hivyo sitaruhusu aondoke bali nitampeleka kituoni.
Wakati namuamuru dereva aende kituoni, akataka aondoke, nikamnyang’anya
funguo ili nimpeleke kituoni,” alisema Koplo Deogratius.
“Ameniita mimi mshenzi, sina akili. Anasema yeye ni mke wa waziri gani?.. Anasema yeye sijui mke wa waziri (anamtaja jina).”
Baadaye
Kamanda Haji anataka aongee na mama huyo ambaye mazungumzo yanaonyesha
anakanusha kumtukana askari huyo, akisema alikuwa akimuomba amuelimishe
dereva kwa kuwa kosa alilofanya ni dogo.
“Mimi sikumtukana, wala
sikumwambia maneno hayo namshangaa sijui leo ameamkaje. Kitu
nilichomuambia kwamba huyu kijana (dereva) alikuwa anakwenda moja kwa
moja, mimi nilikuwa na vihela kidogo nilikuwa nataka kuchenji ili nimpe
fundi,” alisema mke huyo wa waziri.
“Nikauliza kosa gani,
akasema eti kosa lake ni kusimama kwenye zebra crossing. Nikamuambia
sawa, hilo ni kosa la kuelimishwa, lakini sasa wewe unamuandikia kwa
kosa kama hilo? Hilo ni kosa dogo, very minor la kuweza kumuandikia?
Lakini kama unamuandikia andika.”
Kupitia maongezi hayo, RTO Haji alisema kosa hilo ni kubwa na lina adhabu kali.
Kupitia maongezi hayo, RTO Haji alisema kosa hilo ni kubwa na lina adhabu kali.
“Nikusaidie kitu
kimoja, katika makosa mabaya sana mojawapo ni dereva kutoheshimu zebra
crossing. Mahakama inapomkuta mtu na hatia ya kugonga kwenye zebra
crossing, adhabu yake ni jela miezi sita. Haina hata faini, hiyo tunaita
dangerous driving (uendeshaji wa hatari),” alisema Haji na kumtaka
Koplo Deogratius kumuadhibu dereva kwa kosa lake.
Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Koplo
Deogratius alikiri kupambana na mke huyo wa waziri, lakini hakutaka
kuingia kwa undani akisema yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi.
“Ni kweli nilimkamata huyo mama lakini, kwanza tuelewane. Mimi siyo msemaji wa polisi. Kama unataka kesho uje pale kituoni, umuone RTO. Kama akiruhusu mimi nitaeleza kila kitu,” alisema Deogratius akiwa maeneo ya Namanga.
Naye Kamanda Haji alithibitisha tukio hilo, lakini akamuelekeza mwandishi kumuuliza kamanda wa polisi mkoani Kinondoni, Christopher Fuime.
“Ni kweli nilimkamata huyo mama lakini, kwanza tuelewane. Mimi siyo msemaji wa polisi. Kama unataka kesho uje pale kituoni, umuone RTO. Kama akiruhusu mimi nitaeleza kila kitu,” alisema Deogratius akiwa maeneo ya Namanga.
Naye Kamanda Haji alithibitisha tukio hilo, lakini akamuelekeza mwandishi kumuuliza kamanda wa polisi mkoani Kinondoni, Christopher Fuime.
Kamanda Fuime alisemai kuwa Rais Magufuli
ameagiza koplo huyo apandishwe cheo kutokana na kusimamia sheria na
kwamba agizo hilo linafanyiwa kazi.
“Mimi ndiyo natoka Dodoma
kwenye hicho kikao cha Rais na maofisa wa polisi. Hilo ni agizo, sasa
unataka tulipinge? Hayo ni mambo ya utawala, wataangalia wenyewe kama
apewe cheo gani. Kwa sasa yeye ni Koplo, kwa hiyo watajua wenyewe wampe
nini. Afande IGP ndiyo anajua,” alisema Fuime.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment