Jumapili akiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma, Rais Magufuli alitangaza kupunguza kodi ya mshahara kutoka asilimia 11 hadi 9.
Punguzo hilo la PAYE ambalo litaanza kutumika katika mwaka huu wa fedha unaonza Julai mosi, lilitabiriwa na Kikwete, mwaka jana katika maadhimisho ya siku kama hiyo.
Katika hotuba yake, Kikwete alisema kodi ya mshahara imekuwa ikipunguzwa mwaka hadi mwaka katika kipindi cha uongozi wake.
“Tumeendelea kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa wafanyakazi mwaka hadi mwaka.
“Tulikuta kodi ikiwa asilimia 18.5. Sasa imefikia asilimia 12 na mwaka huu tutaendelea kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
Ukiwa mwaka wake wa mwisho madarakani, hakuwa na uhakika wa kufikia kiwango hicho kutoka kodi ya mshahara kuwa tarakimu mbili hadi moja.
“Ndiyo tuko kwenye mchakato wa bajeti sijui kama kweli tutafikia kwenye asilimia tisa ninayosema lakini naamini hatutakuwa mbali sana kama hatutafikia,”alisema na kuongeza:
“Kama tutabakisha patakuwa ni padogo kiasi ambacho naamini kwamba huyo Rais anayefutia atamalizia halafu sifa atapata yeye… kwamba yule mzee tulipiga risala hasikii. Amejitahidi kupunguza, lakini hakufikia pale, wewe umefika asilimia tisa mwaka huo huo.”
Pia Rais huyo mstaafu aligusia suala la kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na kusema kuwa hupangwa na bodi za mishahara ya sekta hizo, ambazo zinaundwa na waziri wa kazi.
“Hadi kufikia mwaka 2011, tulikuwa na bodi za mishahara za kisekta 12, ambazo zimeweza kufanya majadiliano na waajiri na waajiriwa katika sekta binafsi,” alisema Kikwete.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment