Watu
wanne wameuawa katika mapambano na polisi yaliyotokea kwenye mapango ya
Amboni mjini Tamga, eneo ambalo polisi mmoja aliuawa Februari mwaka
jana katika tukio lililohusishwa na ugaidi.
Katika
tukio hilo la Februari mwaka jana, polisi walilazimika kuomba msaada wa
askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kukabiliana na watu waliokuwa
wamejificha kwenye mapango hayo na kupiga kambi hapo hadi
walipokisambaratisha kikundi hicho kilichoelezwa kuwa na sura ya ugaidi.
Mapambano
ya jana yametokea kwenye eneo hilo la kihistoria wakati polisi
wakiendesha operesheni ya kusaka majambazi waliofanya mauaji katika duka
la Central Bakery.
Majambazi
hao walivamia duka maarufu la Central Bakery mwezi uliopita na kuwaua
watu wanne, kujeruhi wawili na kupora Sh2.7 milioni baada ya kufanikiwa
kuvunja kasiki.
Jana
ilikuwa siku ya tatu tangu milio ya risasi ianze kusikika katika
mapango ya Amboni na baadaye taarifa kuenea jijini Tanga kuwa kulikuwa
na majibizano ya risasi.
Kamanda
wa polisi wa mkoa, Leonard Paulo aliwataja waliouawa katika
mashambulizi ya risasi yaliyotokea katika mapango ya Amboni kuwa ni
Nasibu Bakari, Abuu Katada, Abuu Mussa na raia wa kigeni aliyetambulika
kwa jina la Idrisa Berato.
Kamanda
Leonard alisema mbali na kuwathibiti majambazi hao, pia jeshi hilo
limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vinavyosadikika kuwa vilikuwa
vinatumika katika matukio ya ujambazi.
Alivitaja
vifaa vilivyokamatwa kuwa ni vocha mbalimbali za simu 195, majambia
saba, mapanga manne, msumeno mmoja, risasi 17 za shortgun, sare za
mgambo, kofia inayofanana na ya sare za JWTZ na pikipiki mbili.
Alisema
wakati wakiendelea na uchunguzi, watu wanne walikamatwa na waliwataja
wenzao ambao walijificha kwenye mapango hayo na ndipo jeshi likavamia
eneo hilo na kufanikiwa kuua watu wanne na kujeruhi mmoja.
Alisema
Katika majibizano ya risasi, askari wawili walijeruhiwa, akiwataja kuwa
ni Gwantwa Mwakisole, mkaguzi msaidizi wa polisi mkoani Tanga na PC
Charles.
Habari zinaarifu kuwa viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu wako jijini Tanga tangu kutokea kwa mauaji hayo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment