Mabadiliko Ndani ya Kizazi na Athari Zake!

Kizazi kimejengwa na tabaka tatu ambazo ni tabaka la ndani, tabaka la kati na tabaka la nje. Katika hali isiyo ya kawaida hutokea mabadiliko katika tabaka la ndani na kusababisha ugonjwa uitwao ‘Endometriosis’. Ugonjwa huu hutokana na tabaka hilo la ndani kuotea kwa nje ya kizazi.
Tatizo hili huambatana na maumivu ya chini ya tumbo na ugumba. Asilimia sabini ya maumivu hutokea wakati wa hedhi, asilimia ishirini na tano ya wanawake huwa hawana maumivu na hugunduliwa tu kama wana matatizo. 

HISTORIA YA UGONJWA
Ugonjwa huu uligunduliwa zaidi ya miaka elfu nne iliyopita na madaktari wanasayansi maarufu wa kipindi hicho baada ya kugundua baadhi ya wasichana wana maumivu sugu ya chini ya tumbo yanayozunguka kiuno na kuona takriban wanawake wote wenye dalili pia wanakuwa wagumba.
Ugonjwa huu wa ‘Endometriosis’ huwaathiri wanawake wote kuanzia wale watoto wa kike ambao hawajavunja ungo hadi wamama watu wazima waliokwishafunga hedhi, yaani wabibi pia wanaweza kupatwa na tatizo hili, haijalishi rangi wala nchi anayotoka, wala haijalishi kama ameshawahi kuzaa au la.
Yapo baadhi ya matukio haya tayari yameshatokea kwa wanawake wazee na watoto kabla ya kuvunja ungo kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 1999 ingawa zaidi ugonjwa huu huwapata wanawake katika umri wa kuzaa. 

CHANZO CHA UGONJWA
Chanzo halisi cha tatizo hili bado hakijulikani kwamba kwa nini hilo tabaka la ndani la kizazi linaotea nje ya kizazi, linapootea nje ya kizazi hujikita kwenye mirija na vifuko vya mayai. Tabaka linapokuwa nje ya kizazi husababisha kila mwanamke anapofikia kuingia katika siku zake nayo hutoka damu na kusababisha maumivu makali sana. 

DALILI ZA UGONJWA
Mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu kuzunguka nyonga, maumivu huanza kidogokidogo na kuwa makali, husababisha kufunga kupata haja kubwa.
Wakati mwingine maumivu huwa sugu na kusababisha mwanamke apate maumivu wakati wa tendo la ndoa na maumivu ya mkojo au kukojoa mara kwa mara. 

Dalili nyingine ni kutopata ujauzio pamoja na kuumwa na tumbo mara kwa mara. Matatizo ya mkojo na maumivu wakati wa tendo la ndoa na maumivu makali ya hedhi, mwanamke anaweza kuwa mgumba. Dalili ya ugumba ni kujikuta anatafuta ujauzito kwa zaidi ya mwaka mzima bila ya mafanikio. 

MAMBO YANAYOCHANGIA UGONJWA
Hali ya kurithi pia huchangia endapo katika familia au ukoo wapo watu ambao tayari walishagunduliwa kuwa na ugonjwa huu kwani una tabia ya kuzunguka katika vinasaba.
Uchafuzi wa mazingira pia huchangia wanawake kupatwa na tatizo hili hasa uwepo wa kemikali ya ‘Dioxins’ katika mazingira ambayo ni matokeo ya mabaki ya uchafu toka katika viwanda vya karatasi na kwenye madawa ya kuuwa wadudu mashambani au kwenye mifugo.
Pia tatizo la ‘Endometriosis’ linaweza kusababishwa na matokeo ya tabaka hilo la ndani kujikita nje ya kizazi kwa jinsi yoyote ile hivyo siyo vema kufanya tendo la kujamiana wakati wa hedhi. 

UCHUNGUZI
Hufanyika kwa madaktari wa magonjwa ya akina mama katika hospitali za mikoa, vipimo mbalimbali kama ‘Ultrasound’ na ‘Laparoscopy’ vitafanyika na jinsi daktari atakavyoona inafaa.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment