Wakenya Waitibulia SIMBA SC


Omary Mdose, Dar es Salaam
BAADA ya Klabu ya Simba kutangaza kutaka kumsajili straika Mrundi, Laudit Mavugo, mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, nao wameingia kati wakiitaka saini ya straika huyo.

Simba ambayo msimu uliopita ilimkosa Mavugo dakika za mwisho, tayari imeanza mchakato wa kumnasa straika huyo huku ikitajwa Wekundu hao wa Msimbazi wameweka mezani kitita cha dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 100).

Mtandao wa Soka25east.com wa Kenya, umeripoti kuwa, Gor Mahia maarufu kwa jina la K’Ogalo, ipo kwenye mikakati ya kumnasa Mavugo ambaye tayari ametangaza kuondoka Vital’O ya Burundi.

Hata hivyo, Rais wa Vital’O, Benjamin Bikorimana amesema bado anaamini Mavugo ataendelea kuwepo klabuni hapo na kuipigania timu yake kuzidi kupata mafanikio.

Wakati huohuo, Mavugo amenukuliwa akisema: “Nataka kuondoka hapa Burundi na kwenda kucheza soka la kulipwa kwani hiyo ndiyo ndoto yangu.”

Mavugo ambaye aliwahi kuzichezea timu za Kiyovu, AS Kigali na Police FC, huu ni msimu wake wa pili ndani ya Vital’O huku akiwa amefunga jumla ya mabao 60 kwa kipindi chote hicho.
Upande wa Simba kumekuwa na taarifa kuwa kuna uwezekano wa Mavugo kutua nchini muda wowote kuanzia leo kwa kuwa wamefikia pazuri katika mazungumzo yao.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment