SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa, Klabu ya Yanga imekiuka kile ilichoagizwa kufanya na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hivyo kuna hatari ya kuadhibiwa.
Kwa mujibu wa TFF, Yanga ilikiuka maagizo hayo kwani awali walitakiwa kuruhusu kuingiza watazamaji 40,000 pekee kwenye mchezo wao wa Jumanne ya wiki hii dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema awali walikaa kikao na viongozi wa Yanga na kukubaliana kwamba watachapisha tiketi 40,000 huku wakitangaza viingilio vya mchezo huo, lakini baadaye wakabadili mawazo kwa kusema watazamaji wataingia bure uwanjani.
“Tunaomba radhi kwa mtu yeyote aliyekumbwa na kadhia baada ya Yanga kutangaza mchezo wao dhidi ya Mazembe kuwa bure hali iliyosababisha kutokea vurugu kubwa.
“Tumeshangazwa na Yanga kukiuka maagizo ya Caf ambayo yaliwataka kuruhusu watazamaji kutozidi 40,000 ambapo Ofisa wa Caf, Sidio Jose Mugadza raia wa Msumbiji ndiye aliyeagiza baada ya Yanga kutangaza mchezo kuwa bure.
“Kilichotokea siku ya mchezo kila mtu amekishuhudia kwani watazamaji walikuwa zaidi ya waliyotakiwa, hivyo maofisa wa Caf walikuwepo na wameona kila kitu, tuombe Mungu yaje majibu mazuri kutoka Caf kwani kama ikija tofauti kuna hatari ya adhabu kuikumba Yanga,” alisema Malinzi.
Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni Caf iliiondosha timu ya ES Setif ya Algeria katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, kufuatia vurugu kubwa zilizofanywa na mashabiki wake kwenye wao dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Katika hatua nyingine, Malinzi alisema Yanga bado haijalipa gharama za uwanja hivyo wanatakiwa kufanya hivyo haraka huku pia akiongeza kuwa TFF nayo inaidai klabu hiyo fedha za ushuru baada ya kukomboa vifaa vyao kutoka Caf.
Aidha, Malinzi aliongeza kuwa, kuanzia sasa, shirikisho hilo ndiyo litakuwa na majukumu yote ya kusimamia michezo ya kimataifa inayoendeshwa na Caf na Fifa tofauti na hapo awali walipokuwa wakiziachia uhuru klabu kujisimamia wenyewe.
Awali kabla ya mchezo huo, Yanga ilisikika mara kadhaa ikilalamika kuhujumiwa na baadhi ya watendaji wa TFF lakini kwa kauli hiyo inaonyesha msuguano baina ya pande hizo mbili utaendelea.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment