MAGUFULI Anasababisha CCM Wote Tuchekwe

HIVI kama ni wewe, utafanyaje iwapo utatoka matembezini na kupishana mlangoni, na mamako mzazi, naye anakwenda matembezini, huku upande mmoja yuko uchi, kwa sababu pindo la sketi au gauni yake limenasa kwenye mkanda juu ya kiuno?, anaandika Nyaronyo Kicheere.

Utafanyae? Utamwacha hivyo hivyo, mamako mzazi apuyange barabarani, huku sikini taiti na gagulo lake vinaonekana? Utamwacha? Aende nusu uchi mitaani hadi atakapokutana na mwanamke mwenzake atakayemshitua kuvaa vizuri?

Au utajikusuru na kuondoa aibu yote na kumwita “mamaa,” halafu akigeuka ndipo umwambie “mama samahani upo uchi hebu vaa vizuri.”
Tatizo la njia hii ni kwamba mwaka mzima mamako akikuona atakumbuka kuwa unafahamu rangi na mshono wa gagulo na chupi yake.

Na hili ndilo lilitupata siku moja zamani zile za kusoma Chuo cha Uandishi wa Habari cha wakati huo (1991), pale Bungoni, Buguruni wilayani Ilala. Ilikuwa mchana wa saa 8.00 tukiwa katika basi la chuo tayari kwenda kutafuta habari.

Kabla ya basi kuondoka, ghafla akatoka mwalimu wetu wa kiume anatokea ofisini kwake, akielekea darasani kufundisha. Suruali yake kwa mbele ilikuwa haikufungwa zipu na chupi ya zambarau inaonekana.

Wale wenzetu wa kike waliishia kushtuka wakiguna na kushangaa “mamaa, aah jamani, maskini! Lakini kwa upande wetu wanaume, mwenzetu mmoja alipata akili ya ghafla na kutelemka kwenye basi, akamkimbilia na kumshitua kabla hajaingia darasani.

“Samahani mwalimu rekebisha suruali yako kwanza,” mwenzetu yule alimwambia mwalimu. Wasichana walishindwa wakaishia kushangaa tu “jamani, maskini, laah, tufanyeje?”
Lakini wanaume tulikuwa tayari kuondoa aibu na uoga, tukamwambia mwalimu wetu na kumwokoa asiaibike.

Hili ndilo tatizo la watu waoga. Watoto wanashindwa kumwambia baba yao au mama yao avae vizuri iwapo wanamkuta nguo imemvuka. Watoto wa kike wanamwonea aibu baba yao anaaibika na watoto wa kiume wanamwonea aibu mama yao.

Mimi nasema ni vema tukaondoa aibu tukaambizana na wazazi wetu kuliko kuwaacha wakatembea barabarani nusu uchi wakiaibika.
Binafsi, nikigundua mwanangu aliniona natembea nusu uchi, lakini akaniacha niende hivyo hivyo nikaaibike, nitamlaani.

Matatizo kama haya ndiyo yanayowakuta wanachama wa chama chetu – Chama cha Mapinduzi – kwa sasa. Wanamwonea aibu mwenyekiti wetu wa CCM taifa na kuumwacha hivi hivi anaaibika bila kumwambia kwamba anakosea.

Mwenyekiti wetu, John Pombe Magufuli, tangu ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri, kafanya mengi mazuri na mengi mabaya pia. Kwa bahati mbaya sana hakuna hata mtu mmoja kwenye chama chetu wa kumwambia pale anapokosea.

Mfano mmoja, ni vile alivyoshughulikia tatizo la Ukuta wa Chadema. Unaweza kuamini kwamba mwenyekiti anayesisitiza usemi wake wa HAPA KAZI TU, eti kawakatalia Chadema wasimuunge mkono kwa kufanya kazi!

Mwenyekiti wetu, anataka watu wafanye kazi, anataka wananchi wamuunge mkono kwa kufanya kazi, lakini hataki Chadema wafanye kazi, hataki Chadema wamuuunge mkono kwa kufanya kazi!

Sasa kama haya si maajabu ya Musa, ni maajabu ya nani? Ya Firauni? Hebu jiulize, mtu mkubwa sana kama Mkuu wa Nchi, tena mwenyekiti wa chama tawala, namaanisha chama chetu, Chama cha Mapinduzi (CCM), anasisitiza hapa kazi tu, lakini hataki wengine wafanye kazi?

Hivi Magufuli anamaanisha nini anapowapiga marufuku Chadema kufanya kazi? Ina maana hajui kwamba kazi ya mwanasiasa ni kufanya siasa? Hajui kuwa siasa ni pamoja na maandamano?
 

Mwenyekiti wetu hafahamu kwamba kazi ya siasa ni pamoja na kufanya mikutano? Nauliza! Hajui kabisa kama vikao vya ndani maofisini ni sehemu ya siasa na ndiyo kazi yenyewe ya siasa?
Kwa nini viongozi wetu wengine wanamwachia mwenyekiti wetu anaumbuka hivi hivi mitaani, redioni, kwenye runinga na kwenye mitandao?

Wanachama wenzangu wa CCM wanaomwachia mwenyekiti wetu aaibike kwa kutomkosoa wanafanya dhambi.

Hii haina tofauti na kumwonea haya mamako mzazi akatembea uchi mitaani, gauni lake limepinda upande mmoja chupi, sikini taiti na gagulo lake vinaonekana kwa wote badala ya kuonekana kwa babako pekee. Ni makosa.

Ondoa aibu umwambie mamako kama yuko uchi na kumwokoa. Mtoto wa kike ondoa aibu na umwambie babako kama yuko uchi na kumwokoa asiaibike mitaani. Hivyo hivyo kwa wanachama wenzangu wa CCM tuondoe aibu na kumwokoa Magufuli asiaibike.

Ni aibu mbele za wananchi wote na watu wa mataifa mbalimbali wanaosikia kaulimbiu ya hapa kazi tu, lakini mwenye kaulimbiu hiyo hataki watu wasio wanaCCM wafanye kazi!

Makada wenzangu wa CCM, wakuu wa mikoa wa zamani na wa sasa; na hata waliotumbuliwa hivi karibuni mkikutana na mwenyekiti Magufuli mwambieni kuwa kazi ya wanasiasa ni pamoja na kufanya mikutano na maandamano.

Makada wenzangu wa CCM waambieni wakuu wa wilaya wa zamani na wa sasa na hata wale waliotuumbulliwa hivi karibuni, kwamba wakikutana na Mmwenyekiti wetu Magufuli wamwambie kazi ya siasa ni pamoja na kufanya vikao vya ndani.

Viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) na Jumuiya ya Wanawake (UWT), Umoja wa Wazazi Tanzania (TAPA), pelekeni ujumbe Ikulu kwamba kiongozi wetu anaaibika. Viongozi wa Jumuiya za CCM jikusanyeni mumwendee Magufuli na kumwelimisha.


Nimelazimika kuandika haya kwa sababu huko mitaani sisi makada wa CCM tunaonekana kama hamnazo. Tukiulizwa kama kazi ya mwanasiasa ni nini tunashindwa kujibu.
Tukisema kazi ya mwanasiasa ni kufanya siasa, tunaulizwa siasa ni nini kama siyo kumwaga sera kwenye maandamano, mikutano na makongamano.

Sasa mahafali au graduation za wanachuo wanachama wa Chadema zimezuiwa, kisa hapa kazi tu, eti twende tukafanye kazi. Mikutano ya Chadema imezuiwa, kisa hapa kazi tu, eti twende tukafanye kazi. Ni kazi ipi? Magufuli hajui kweli maana ya siasa?

Sasa sisi sote ndani ya CCM tunaonekana hatujui Kiswahili. Hata neno moja tu la Kiswahili la siasa hatujui maana yake. Wote makada wa CCM, wanachama na wafuasi, hatujui maana ya neno siasa la sivyo tungemwelimisha mwenyekiti wetu.

Makada tunataniwa kuwa ni Wasukuma wa Nyanshimo hatujui Kiswahili. Chadema waachiwe waandamane, wafanye mikutano na wafanye vikao vya ndani. Ndiyo kazi yenyewe hiyo ya siasa. Hii itatuondolea aibu.

Leo mitaani tunataniwa eti ndiyo kawaida yetu hatujui Kiswahili kama yule kada wetu mmoja aitwaye Wassira aliyemtwanga mwandishi ngumi kwa kumwambia eti ni swahiba wa fulani, hakujua maskini kwamba swahiba ni rafiki.
Chanzo: Mwanahalisionline
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment