Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishindana peke yake Machi 20, 2016, halafu kinadai kwamba kilishinda kwa kishindo!
Wakati Shein akisema hivyo, Balozi Seif Ali Iddi, msaidizi mkuu wake, alipokuwa akizungumzia uchaguzi wa marudio wa Machi 20, alisema, “Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaendelea kuwapo.”
Machi 20 tulioneshwa vituo vingi vya kura kote Unguja na Pemba vikiwa bila wapiga kura. Tulishuhudia – kupitia mitandao ya kijamii – picha za wapiga kura wachache walioshiriki wakifanya vituko kwenye vyumba vya kura.
Kuna waliopewa karatasi zaidi ya moja za kura. Wapo walioandika, “Allah Akbar” – Mungu Mkubwa – kwenye karatasi za kura.
Wapo waliomtumia ujumbe wa simu na video Jecha Salum Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), na kumwambia, “Jecha, tambua kuwa dhuluma haidumu!”
Ingawa walipanga uchaguzo huo kama njia ya kukomoa Chama cha Wananchi (CUF), yaliyotokea, ingawa yamemrudisha Dk. Shein madarakani, yamedhalilisha CCM na watawala wanaong’ang’ania madaraka.
Lakini sikio la kufa huwa halisikii dawa! Mtumiaji mmoja wa mtandao, ambaye kwa hakika ni mwana-CCM aliyekwenda kupiga kura kwa hiyari yake, aliniandikia hivi:
“Nimeondoka nyumbani kwangu Mwembenjugu saa 8:00 mchana kwenda kupiga kura kituo cha Kidongo Chekundu na saa 8:30 nikawa nisharejea nyumbani. Hii unajuwa maana yake ni nini, Mohammed?”
Nikamjibu, “sijui.” Akaniambia, “inamaanisha kuwa hata sisi wana-CCM tumegomea uchaguzi huu. Hapa Mwembenjugu, Sogea, Kwahani, Kidongo Chekundu pote hapa ni CCM watupu. Lakini vituo vilikuwa vitupu.”
Ndiyo maana bado tunatilia shaka matokeo yaliyotangazwa na kumpa Dk. Shein kura 299,982 sawa na asilimia 91.4 ya kura. Haya ni mazingaombwe.
Dk. Shein anafahamu kuwa Wazanzibari hawajakataa SUK, bali wamemkataa yeye. Mara ya kwanza walifanya hivyo tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kumnyima kura na kuchagua mwingine.
Kwa watawala kukataa matokeo ya 25 Oktoba 2015, walikuwa wanatoa fursa ya pili kwa wananchi kumkataa Dk. Shein.
Maneno haya yanayotolewa na Dk. Shein, ni vijembe tu vya kisiasa vinavyotokana na ukweli anaijua, na vinavyothibitisha ukweli huo kwamba naye anajua kuwa wananchi walimkataa.
Ukweli kwamba amemteua Balozi Seif Ali Iddi kuwa makamu wa pili, unatumia mantiki kuwa kulitakiwa awepo makamu wa kwanza, maana huwezi kuwa na wa pili bila ya kuwa na wa kwanza.
Lakini kwa kuwa umma umemkataa Dk. Shein, hawezi kupata makamu wa kwanza kikatiba. Atabaki kuwa na makamu wa pili bila makamu wa kwanza.
Nakumbuka tarehe 25 Oktoba 2015 pale Bungi Miembe Mingi, Wilaya ya Kusini Unguja, baada ya Dk. Shein kupiga kura, waandishi wa habari walimuuliza kwa nini alikuwa anaamini Wazanzibari wangekuwa na sababu za kumchagua tena kuwa rais wao. Alitaja sababu kadhaa, lakini kubwa yote alisema ni mafanikio yake kwenye kuongoza SUK.
Akajisifia kuwa hata mataifa ya nje yanakuja Zanzibar kujifunza namna Wazanzibari walivyoweza kujenga na kuendesha serikali hiyo. Akamalizia kuwa chochote kizuri ambacho alikuwa amefanya kwenye miaka ile mitano ya awali ya uongozi wake, kilitokana na ushirikiano wa pande zote mbili – CUF na CCM; na kwamba kama kuna makosa, wamekosea pamoja.
Mtu yule yule aliyejinadi kwa jina la SUK, leo miezi mitano baadaye, anajitapa kwa kuvunja SUK.
Anafanya hayo akiwa na kumbukumbu kuwa katika kipindi cha 2010-2015, yeye alikuwa kiongozi wa Serikali ya Zanzibar asiyekubalika kwa wananchi na asiyepata heshima stahiki kutoka kwa wenzake. Aliweza kukaa madarakani kwa sababu tu ya roho ya mapatano ndani ya SUK.
Sasa kwa kuwa amekataliwa, akalazimisha kubaki madarakani, uongozi wake utakumbana na mambo mawili.
Hatakubalika na hataheshimika. Ametwaa madaraka kwa vitisho na dhuluma; kwa kuamini nguvu yam tutu kuliko nguvu ya kura.
Wenzake wanajua, na yeye anajua kuwa maisha ya kisiasa aliyojichagulia ni kitanzi kwake mwenyewe na chama chake.
Makala hii imeandikwa kwenye gazeti la MSETO wiki hii.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment