John Magufuli, Rais wa Tanzania akioneshwa ramani ya barabara za juu zitakazojengwa kwenye makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, Tazara
Rais John Magufuli leo ameweka jiwe la msingi kwenye uzinduzi wa barabara za juu kwenye makutano ya Barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara jijini Dar es Salaam.
Ameweka jiwe hilo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo ikiwa ni sehemu ya makakati wa kupunguza foleni zilizokuwa zikipigiwa kelele na Ukawa bungeni.
Viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakilalamika kuhusu matatizo ya foleni Dar es Salaam huku wakitoa mawazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za juu.
James Mbatia (NCCR), Mbunge wa Vunjo, Kilimanjaro mwaka 2013 akiwa Mbunge wa kuteuliwa, aliwahi kusema kuwa, tatizo la msongamano wa magari hulisababishia taifa hasara ya takriban Sh1.46 trilioni kwa mwaka.
Uzinduzi huo uliofanywa kwa mara ya kwanza katika Jimbo la Temeke linaloongozwa na Abdallah Mtolea kutoka Chama cha Wananchi (CUF), unalenga kuanza kutatua tatizo la msongamano wa magari jijini humo na mengine yanayotokana na foleni.
Mwaka 2013 utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saikolojia na Tabia za Watu ya nchini Marekani, ulibainisha kuwa, foleni huchangia kwa kiasi kikubwa kusababisha maradhi ya akili yanayoweza kujitokeza baada ya miaka10 ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo.
Utafiti huo pia uliungwa mkono na Modester Kimonga, Mtaalamu wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dodoma, aliyesema kuwa kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu husababisha hasira, hatimaye msongo wa mawazo.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo na utagharimu Sh. 100 bilioni Rais Magufuli ameeleza kuwa, ujenzi huo utaanza hivi karibuni kwa ushirikiano na Serikali ya Japan.
Amesema, serikali ya Japan imefadhili mradi huo kwa Sh 93.44 bilioni wakati serikali ya Tanzania imechangia Sh 8.36 bilioni.
Akizungumzia ajira zitakazopatikana kutokana na ujenzi huo, Rais Magufuli ametoa raia kwa wananchi watakaopata ajira kuwa waaminifu sambamba na kutunza vifaa vya ujenzi.
“Serikali ya Awamu ya Tano imetenga shilingi Trilioni Moja trilioni kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kwa reli ya kati,” amasema Rais Magufuli na kuongeza;
“Tutajenga kituo kikubwa Ruvu ili mizigo isafirishwe kwa njia ya reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Ruvu na malori yatakuwa yakichukua mizigo pale, jambo hili litasaidia kupunguza foleni hapa Dar es Salaam.”
Kwenye uzinduzi huo Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Japan kutokana na ufadhili huo na mingine kwa zaidi ya miaka 36 sasa.
Hata hivyo, Rais Magufuli ameonesha kukerwa na misaada iliyo na masharti magumu “ni bora kula muhogo wa kujitafutia kuliko kula mkate kwa masimango.”
Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kujenga barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na barabara za juu tano.
-mwanahalisi
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment