KIIZA Atimuliwa Kambini, SIMBA SC



Mshambuliaji wa Simba, Hamisi Kiiza.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam PAMOJA na uwezo wake wa kupachika mabao, lakini sasa vituko kwa mshambuliaji Hamisi Kiiza wa Simba imekuwa ni “bandika bandua”.
Uongozi wa benchi la ufundi la Simba, umemtimua kambini mshambuliaji huyo mwenye mabao 19 baada ya kutotimiza utaratibu wa timu kama ilivyokuwa imeagizwa na Meneja wa Simba, Abbas Ally ‘Gazza’.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, raia wa Uganda, aliondolewa kambini Dege Beach, juzi baada ya kuonekana alifanya ujeuri kwa kutovaa sare kama wenzake wakati kikosi cha Simba kilipofunga safari kwenda Uwanja wa Taifa kuishuhudia Yanga ikicheza na Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Awali, taarifa zilieleza kuwa Kiiza alilumbana na Kocha Jackson Mayanja, lakini kocha huyo akafafanua jana jioni.
“Si mimi, nafikiri watu wanapotosha, Kiiza alitakiwa kuvaa sare na pia kutumia basi la timu akakataa. Akaja na nguo zake za kawaida pia akitumia gari lake. Hivyo meneja akaona si sahihi akamuondoa kambini.

“Hili ni kati ya Kiiza na meneja, hata wakati wanapanga mimi sikuwepo. Sasa kama amekosea, meneja ameamua na mimi nitabaki kwenye msimamo wa benchi la ufundi, lakini hajazozana na mimi,” alisema.

Hata hivyo, kumekuwa na taarifa, kwamba Mayanja ameamua kumtupa benchi yeye pamoja na beki Juuko Murshid kwa kuwa walichelewa kurejea kambini na hawako fiti. Tayari uongozi wa Klabu ya Simba uliwaandikia barua wawili hao kuwataka kujieleza kutokana na kuchelewa huko.
“Hilo la kucheza au kutocheza, libaki kuwa kazi ya benchi la ufundi, hatuwezi kutangaza kila kitu,” alijibu Mayanja kuhusu kucheza kwao au la.
Kiiza amemueleza rafiki yake wa karibu ambaye amezungumza na Championi Jumatatu kwamba alikuwa na kikao na mmoja wa viongozi wa Simba.

“Alikwenda kwenye kile kikao, tena alikuwa na Kassim Dewji waliyekuwa wakizungumza masuala ya timu. Alichelewa kutoka sasa asingeweza kuwahi basi au kuvaa sare kama wenzake. Hilo likamuudhi meneja lakini si kosa la Kiiza hata Dewji alizungumza nao, huenda yeye alifanya kosa kuwataarifu benchi la ufundi,” alieleza rafiki yake huyo.

Pia imeelezwa, wachezaji wenzake walionekana kukerwa na hilo na jana asubuhi kilifanyika kikao kuwapoza na kuwaeleza kwa nini Kiiza arudishwe kambini kwa kuwa aliyemchelewesha ni kiongozi.
Juhudi za kumpata Kiiza hadi jana jioni ziligonga mwamba kwa kuwa hakuwa akipokea simu lakini inaelezwa tayari amerejea kambini Dege Beach akiwa na wenzake, lakini mechi ya leo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Coastal Union, hatacheza.

Huu ni msimu wa kwanza wa Kiiza Simba, lakini hili ni tukio lake la tatu linalohusiana na nidhamu baada ya kuanza na lile la kumtetea Hassan Isihaka mtandaoni licha ya kujua alifanya utovu wa nidhamu.
Siku chache baadaye akaingia kwenye sakata la kuchelewa kurejea kambini kwa zaidi ya siku tano, hilo halijaisha, hili ni la tatu na utagundua matatizo mara mbili dhidi ya uongozi na hili ni dhidi ya benchi la ufundi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment