Serikali imeanzisha mpango maalumu wa mafunzo kwa wahitimu kutambua
ujuzi katika sekta zisizo rasmi, ili kuwajengea vijana wigo mpana wa
ajira kwa fani walizosomea.
Mpango huo unalenga kutoa mafunzo ya
ufundi katika fani mbalimbali kwa vijana walioishia darasa la saba,
kidato cha nne au sita na wanaohitimu vyuo mbalimbali.
Lengo ni kuwawezesha vijana kupata ajira na waajiri nao kupata watu wenye ujuzi wa kutosha.
Akizungumzia
mpango huo juzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ajira Ofisi ya Waziri
Mkuu, Robert Masingiri alisema changamoto kubwa kwa vijana ni ukosefu
wa ajira hasa wanaomaliza shule bila kuwa na fani yoyote.
Masingiri
alisema baada ya Serikali kuona upungufu huo, imeandaa mpango maalumu
unaofadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kutoa mafunzo kwa
vitendo kwa wanafunzi na wahitimu wa vyuo mbalimbali.
“Licha ya
kutoa mafunzo hayo, tutatambua ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi.
Tutawapa wataalamu hao baada ya kukaa nao na kuona uwezo wao, hiyo
itawasaidia kupata ajira hasa zinapokuja kampuni za uwekezaji au
viwanda,” alisema.
Masingiri aliongeza kuwa nia ya Serikali ni
kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi ambao wako kazini, mpango huo utaanza na
vijana 5,000.
Mkurugenzi wa ILO nchini, Mary Kawar alisema
Tanzania imefanikiwa kuandaa mpango utakaosaidia vijana wengi kupata
ajira
“Kwa muda mrefu kumekuwa na pengo kati ya elimu ya darasani na
utendaji. Naamini mafunzo haya yatatoa fursa ya pekee kuziba pengo hilo
na kuongeza sifa za kuajiriwa,” alisema Kawar.
Mkurugenzi wa
Taarifa za Soko la Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ahmed Makbel alisema
mpango huo utakuwa na manufaa kwa waajiri na waajiriwa, kwa sababu wote
watapata wanachohitaji.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment