Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (Alat), wanaotokana na
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesusia
uchaguzi kwa madai ya kuminywa kwa demokrasia.
Mkutano huo
uliofanyika jana katika ukumbi mpya wa CCM mjini Dodoma, wajumbe wake ni
wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri zote, mameya wa miji na majiji
na mbunge mmoja kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara.
Nafasi zilizokuwa zikigombewa ni mwenyekiti, makamu wake na wajumbe 16 wa kamati ya utendaji.
Awali,
Mwanasheria wa Alat, Cleofas Manyangu aliwataja waliochukua na
kurejesha fomu za kugombea uenyekiti ni Gulam Mukadam (Meya wa
Shinyanga), Murshid Ngeze (Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba
Vijijini), Chief Kalumuna (Meya wa Bukoba Mjini) na Isaya Charles (Meya
wa Jiji la Dar es Salaam).
Hata hivyo, alisema waliokidhi vigezo
kwa mujibu wa Katiba ya Alat, kanuni za kudumu na mwongozo ni Mukadam
na Ngeze wote kutoka CCM na waliosalia wa Ukawa hawakukidhi.
Alisema
Charles na Kalumuna walishindwa kurejesha fomu katika muda uliowekwa wa
saa 6.00 mchana siku moja kabla ya uchaguzi na pia hawakupata wadhamini
10 kutoka kanda tano za Alat Taifa.
Kutokana na kauli ya
mwanasheria huyo, mwenyekiti wa muda wa mkutano huo ambaye pia ni Meya
wa Manispaa ya Dodoma, Jaffar Mwanyemba alitangaza kuwa wagombea katika
uchaguzi huo ni wawili.
Kauli hiyo ilibadilisha hali katika
ukumbi, huku wajumbe wa Ukawa wakitaka wagombea wote waruhusiwe kuingia
katika kinyang’anyiro hicho.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist
Lazaro aliomba wagombea hao waruhusiwe kwa kuwa maandalizi ya uchaguzi
yalikiuka mwongozo, hali ambayo ilifanya baadhi yao kutokidhi vigezo.
Alisema
taarifa ya mkutano huo ilitakiwa kuwafikia siku zisizopungua 28 kabla
ya uchaguzi, lakini wengi wao walipata barua hizo chini ya muda huo.
Akijibu
hoja hizo, Manyangu alisema taarifa za mkutano huo kwa mara ya kwanza
zilipelekwa kwenye halmashauri Novemba 2, mwaka jana.
“Tatizo
lililotokea ni baadhi ya halmashauri kuchelewa kukamilisha uchaguzi,
hali iliyosababisha mkutano kuahirishwa mara mbili,” alisema.
Baada
ya hoja hizo, wajumbe wote wanaotokana na Ukawa walitoka nje ya ukumbi,
huku wakiahidi kufanya kazi na Serikali Kuu pekee.
Akizungumza
nje ya ukumbi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles alisema kutokana
na kuchelewa kwa uchaguzi jijini humo hakupata taarifa mapema kuhusu
mkutano na uchaguzi huo.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini
(ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe na meya wa Manispaa ya Kigoma walishiriki
uchaguzi kama kawaida.
“Mimi sijui chochote. Sijui wametoka kwa sababu gani maana nimefika hapa nikiwa nimechelewa,” alisema Zitto.
Katika
uchaguzi huo, Mukadam alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kura 179 kati ya
276 na makamu wake ni Stephen Muhapa aliyepata kura 152 kati ya 272.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment